Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Julius S. Mtatiro, amefanya ziara ya kawaida ya kukagua uendeshaji wa maghala ya kuhifadhia korosho katika wilaya hiyo Disemba 22, 2023.
Ziara hiyo iliyoambatana pamoja na kamati ya Ulinzi na Usalama, Chama Kikuu cha Ushirika, wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, ilifanikiwa kutembelea maghala 7 yaliyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Tunduru ambayo yanahifadhi Korosho.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, kuelekea mnada wa Mwisho wa zao la Korosho Wilayani Tunduru,Mhe. Mtatiro aliagiza kuundwa Kwa kamati ndogo ya wataalamu ili kuendelea kukagua na kuhakikisha kuwa maghala yote 7 yamezingatia miongozo ya kuhifadhi na kusafirisha korosho katika magunia yenye ujazo si chini ya kilo 80, ambapo hii itasaidia kulinda ubora wa soko la zao hilo na kuongeza thamani yake.
Mhe, Mtatiro amesisitiza, kuendelea kulinda uchumi wa zao hili kwa kuhakikisha kuwa korosho zinasafirishwa kwa njia sahihi na zinapelekwa kwa wanunuzi zikiwa katika ujazo na ubora unaohitajika na wanunuzi wa zao hilo.
“Korosho ni zao muhimu sana la biashara nchini Tanzania, linasaidia kuingiza fedha nyingi za kigeni, hivyo, yatupasa kulisimamia kwa kufuata miongozo iliyopangwa ili kuweza kulinda ubora wake”. Alisisitiza.
Akiwa katika ziara hiyo, Mhe. Mtatiro alipata wasaa wa kuzungumza na watendaji pamoja na wenyeviti wa vyama vya msingi (AMCOS) ambapo Mhe, Mtatiro, alisisitiza umuhimu wa AMCOS kuwalipa wakulima kwa wakati, kwani itasaidia kuongeza motisha kwa wakulima kulima korosho kwa wingi.
Aidha Mhe. Mtatiro amepongeza vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) ambavyo vimekuwa vikichapa kazi vizuri katika kuhifadhi na kusafirisha korosho, amewataka vyama hivyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kuwa korosho za Tanzania zinapata soko la uhakika na wakulima wanapata bei nzuri.
Katika ziara hiyo, watendaji nane katika maghala matatu walishikiliwa na vyombo vya usalama Kwa ajili ya maelezo zaidi, kwasababu ya kutoonesha uaminifu katika utunzaji na usafirishaji wa zao hilo kwenda kwa wanunuzi
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.