Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Denis Masanja, leo amezindua rasmi zoezi la ugawaji wa madawati 939 mapya kwa shule za msingi na sekondari zilizopo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.

Pichani: Mhe.Masanja akikabidhi Madawati kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Muungano.
Madawati hayo yametengenezwa kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri yenye thamani ya shilingi milioni 103.3.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Masanja amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, pamoja na kupunguza changamoto ya uhaba wa madawati shuleni. Ameeleza kuwa usimamizi mzuri wa mapato ya ndani ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo ya haraka na ya moja kwa moja kwa wananchi, hususan katika sekta ya elimu.
Mhe. Masanja amepongeza uongozi wa Halmashauri, wataalamu pamoja na wananchi kwa ushirikiano wao katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, akisisitiza kuwa mafanikio hayo ni ushahidi wa wazi kwamba mapato ya ndani yakisimamiwa kwa uadilifu yanaweza kutatua changamoto nyingi zinazowakabili wananchi.
Aidha, amewataka walimu na wanafunzi kuyatunza madawati hayo ili yadumu kwa muda mrefu na kuendelea kuwahudumia wanafunzi wengi zaidi.
Zoezi la ugawaji wa madawati linaendelea katika shule mbalimbali ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru,ambapo kwa awamu ya kwanza madawati 378 yataenda katika shule 16 , ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kila mwanafunzi anapata mazingira bora, salama na rafiki ya kujifunzia.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.