Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Denis Masanja, amefanya kikao na watumishi wa idara ya afya ambapo amewataka kuwa wajibu, kujitolea, na kuwatumikia wananchi kwa uaminifu na weledi wa hali ya juu. Kikao hicho kililenga kuboresha huduma za afya katika wilaya ya Tunduru.

Katika hotuba yake, Mhe. Masanja alisisitiza masuala mbalimbali muhimu yanayohusu utoaji wa huduma bora. Alianza kwa kusisitiza umuhimu wa uwajibikaji na utoaji wa huduma bila kuchelewa. "Kila mmoja awajibike, tujitoe. Tumekuja kuwatumikia wananchi. Hatutaki kusikia manungāuniko ya kuchelewa kutoa huduma Pamoja na changamoto zinazoweza kusababishwa na mtandao na mfumo bado tujitahidi kuhakikisha tunatoa huduma kwa haraka bila kuchelewa wakati tukitatua changamoto hizo" alisema.
Vilevile, aligusia suala la usalama wa taarifa za wagonjwa, akisisitiza kuwa ugonjwa ni siri kati ya mgonjwa na muuguzi wake. "Nina Imani Usalama wa taarifa za wagonjwa utazingatiwa muda wote," alieleza.
Mhe. Masanja pia alisisitiza suala la usafi wa mazingira ya vituo vya afya, akisisitiza kuwa ushiriki wa watumishi katika zoezi la usafi ni jambo la lazima. Kuhusu mavazi, aliwataka watumishi kuvaa kwa kufuata miongozo iliyowekwa ili kuleta heshima na utambulisho wa taaluma.
Ili kuboresha utoaji wa huduma na kujitathmini, Mhe. Masanja alitoa maelekezo ya kuanzishwa kwa kitengo cha kupokea malalamiko na kuweka masanduku ya maoni. Alisema hatua hii itasaidia kujua kiwango cha kuridhika kwa wananchi na huduma zinazotolewa. "Hii itatusaidia kujua kiwango cha utoaji huduma na kujitathmini," aliongeza.
Akizungumzia suala la upatikanaji wa dawa, Mkuu wa Wilaya alisisitiza kuwa malalamiko ya wananchi kuhusu ukosefu wa dawa yanapaswa kushughulikiwa haraka. Aliongeza kuwa ni muhimu kuweka mikakati ya utoaji elimu kwa wananchi kuhusu Magonjwa ya mlipuko na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza kama vile Kipindupindu, Mpox, Kisukari, Magonjwa ya moyo na shinikizo la damu na mengineyo.

Mhe. Masanja alikumbusha kuwa Wilaya ya Tunduru ina changamoto ya mwingiliano mkubwa wa watu kutokana na eneo lake la mpakani, barabara kuu, uchimbaji wa madini, na kilimo cha mikakati. Hali hii inahitaji weledi na umakini wa hali ya juu katika kutoa huduma za afya.
Mwisho aliwapongeza kwa huduma nzuri za Afya wanazotoa na kuwataka kuzingatia maelekezo yake ili tuendelee kutoa huduma bora kwa wananchi.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.