Na Theresia mallya –Tunduru
12/05/2019
Katika kupunguza tatizo la wanafunzi kutembea umbali wa zaidi ya kilomita moja kutoka kijijini hadi shule ilipo wananchi wa kijiji cha Mindu kilichopo Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wazazi wameshiriki ujenzi wa vyumba 5 vya madarasa na ofisi ya walimu moja.
Akisoma taarifa ya Kata ya Mindu kwa mkuu wa wilaya Juma Zuberi Homera mtendaji wa Kata ya Mindu Ndg William Charles Mngwira alisema kuwa watoto wamekuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilomita moja kwenda shuleni hali inayohatarisha usalama wao hasa wale wa darasa la awali na darasa la kwanza hadi tatu, na kwa watoto wa kike.
Kutokana na adha hiyo alisema kijiji cha Mindu kilichokuwa kikitumia shule iliyotumika toka kipindi cha ukoloni iliyojengwa mwaka 1936 kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya upili, (Middle Class) kumeleta changamoto kwa watoto kuwa na utoro wa rejareja, mahudhurio hafifu, baadhi ya watoto kuacha shule na kukosekana kwa usalama wa watoto.
Serikali ya kijiji kwa kushirikiana na wazazi wameamua kuanzisha ujenzi wa madarasa 5 kwa nguvukazi za wananchi na fedha iliyotumika ni shilingi 11,880,000/=, ambapo mbunge wa Tunduru Kaskazini Eng Ramo Makani alitoa mchango wa milioni 5.
Madarasa haya yaliyojengwa katika makazi ya wananchi yapo katika hatua ya kuezeka, ambapo jumla ya bati 270 zinahitajika ili kukamilisha ujenzi huo na kuondokana na tatizo la watoto kutembea umbali mrefu kufata huduma ya elimu.
Aidha taarifa iliendelea kusema kuwa Kata hiyo yenye wakazi zaidi ya 7000 haina sekondari ya Kata hivyo kukamilika kwa ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi yaliyokaribu na makazi ya wananchi kutatoa fursa ya ukarabati wa majengo ya iliyokuwa shule ya msingi Mindu kuwa shule ya sekondari.
wananchi wa kijiji cha mindu wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera kwenye mkutano wa hadhara ambaye hayuko kwenye picha.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe. Juma Zuberi Homera alianza kuupongeza uongozi wa kata, kijiji, shule wananchi wote wa Kata hiyo kuona umuhimu wa watoto wao na kuanzisha ujenzi wa majengo ya shule ya msingi Mindu katika makazi ya kijiji kwani itaongeza morali kwa watoto kupenda shule zaidi.
Mkuu wa wilaya hiyo alisema kuwa ametembelea eneo la ujenzi na kuona kazi nzuri inayofanywa na wananchi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa,pia alipata fursa ya kufika kwenye shule wanayosoma watoto kwa sasa ambayo ni mbali sana kutoka kijijini hadi kufika shuleni hivyo sio salama kwa watoto hasa wale wadogo wa madarasa ya chini.
“Nimeona juhudi zenu katika kumaliza changamoto ya wanafunzi kutembe umbali mrefu kwa kujenga majengo ya shule ndani ya mazingira ya kijiji, na katika taarifa nimesikia kuna changamoto ya kumalizia ujenzi huo kwa kukosa fedha ya kununua bati”alisema mkuu wa wilaya.
Aidha Mhe.Juma Zuberi Homera alipata fursa ya kuendesha harambee kwa wadau wa maendeleo wilayani Tunduru ili kupatikana kwa bati 270 zinazohitajika katika kuezeka majengo hayo ili yaanze kutumika hadi ifikapo disemba 2019.
Katika harambee hiyo iliyoendeshwa na mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera kwa wadau wa maendeleo wa wilaya ya Tunduru,wadau walitoa ahadi ya kuchangia bati 161 ikiwa ni pamoja na mkuu wa wilaya kuchangia Bati 55 kuunga mkono juhudi za wananchi.
muonekano wa vyumba vya madarasa yanayojengwa kwa nguvu za wananchi na mchango wa mfuko wa jimbo Tunduru kaskazini ili kuondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shuleni wanakosoma kwa sasa.
Juma Homera alisema “katika kata ya Mindu nimafanya mambo mengi sana ikiwa ni pamoja na kutoa michango ya bati 5 za kueezeka matundu ya choo shule ya mingi Mtonya, saruji mifuko 50 shule ya msingi Mjimwema na fedha taslimu laki tano (500,000) shule ya msingi Liwangula lakini niwaombe wazazi wa Mindu kuwachangia watoto chakula shuleni ili watoto wasome kwa utulivu na kusoma katika mazingira rafiki”
Na kwa upande saimon Ambul Simbuya mkazi wa kijiji cha Mindu alisema kuwa watoto wanapata adha sana kutembea umbali mrefu kutoka kijijini kwenda shuleni ambapo hali hii hatari sana kwa watoto wadogo hasa kipindi cha mvua na ni raisi hata kukutana na wanyama wakali njiani.
Saimon simbuya alieleza kuwa kata yao ya Mindu haina shule ya sekondari hali inayoadhiri watoto wanaofaulu kutoka shule za kata hiyo kwenda shule ya kata jirani, hivyo kukamilika kwa majengo ya shule wanayojenga kutarahisha kwani watafanya ukarabati wa madarasa ya shule inayotumika kwa sasa kuanzisha shule ya sekondari.
“wanafunzi wengi wa kike wa sekondari kutoka Kata ya Mindu wanakatiza masomo kutokana na kwenda kusoma katika shule ya kata jirani sekondari ya Mtutura na kuishi mtaani kwa kujitegema hivyo hupata mimba na kuacha masomo, kuanzishwa kwa sekondari tutapunguza tatizo na kupata wasomi wengi katika kata yetu”alisema bw. Simbuya.
Naye mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mindu alisema kuwa kumekuwa na tatizo la utoro kwa wanafunzi hasa kipindi cha mvua unaochangiwa na umbali, wanafunzi kuchelewa shuleni na pia utoro unachangiwa kwa kiwango kikubwa na ukosefu wa chakula shuleni endapo watoto watakua wanapata chakula cha mchana shuleni tatizo hili litapungua.
Lakini uongozi wa shule uliona changamoto hiyo hivyo ikaamua kushirikiana na serikali ya kijiji kujenga madarasa katika makazi ya kijiji ili kuondoa na kuamaliza kabisa tatizo hili na kujenga jamii yenye weledi kwani vijana wetu wakiacha shule wengi tutatengeneza taifa ambalo ni mbumbumbu na ile haki ya elimu kwa kila mtoto haitofikiwa.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru amekuwa ni chachu kubwa sana katika kuchangia maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na maji, afya, elimu na nyingine ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma kwa wakati na kujikwamua kiuchumi na kufikia mafanikio ya maendeleo endelevu ifikapo 2025.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.