Asasi ya kiraia COUNSENUTH ambao ni wasimamizi wa utekelezaji wa mradi wa Kijana Jiongeze kwa kushirikiana na Halmashauri kupitia ufadhili wa MasterCard Foundation imefikia tamati kwa awamu ya pili ya mradi huo, huku wakikabidhi vifaa vya michezo na taaluma (Kamusi na Jezi) ili kuendelea kuinua sekta ya michezo pamoja na Elimu kwa shule 23 za Sekondari zilizopo Wilayani Tunduru.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mheshimiwa Simon Chacha ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliipongeza asasi hii kwa kuendelea kuwa miongoni mwa wadau ambao wanameweza kusaidia kuinua Sekta ya Elimu katika Wilaya ya Tunduru.
“Niwapongeze kwa kuweza kumaliza awamu yenu ya pili ya mradi huu wa Kijana Jiongeze, pamoja na mafanikio tuliyonayo kama Wilaya katika sekta hii ya Elimu, lakini bado tunawahitaji, tutashukuru sana kama mkiendelea kuwa nasi kwa awamu nyingine tena” Alisema “Tunawashukuru kwa kuwa mchango mkubwa katika kuinua ufaulu wa wanafunzi wetu”.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya kiraia COUNSENUTH Bi. Shakila Mayumana ameeleza kuwa, wameweza kupata mafanikio makubwa kupitia mradi huu, ikiwemo kuongeza ufaulu katika Shule ambazo walizifikia, kupunguza utoro wa wanafunzi, wameweza kusaidia watoto kujitambua na pia wameweza kuanzisha bustani za mboga mboga na matunda, kuhamasisha michezo na vile vile mradi huu umewezesha kuanzishwa na kuboreshwa klabu mbalimbali zilizoko mashuleni kwa mfano Kijana Jiongeze, klabu za Ushauri wa kitaaluma (Career guidance and councelling Club), kuboresha mahusiano kati ya mwalimu na mwanafunzi, pamoja na kuongeza ushiriki wa wazazi hasa kwenye masuala ya elimu.
Aidha, Bi. Shakila alitumia fursa hiyo kuwaomba Walimu, Halmashauri na Wilaya kwa ujumla kuendeleza shughuli na mafanikio yaliyoletwa na Mradi wa Kijana Jiongeze ili uwe endelevu.
Mradi wa Kijana Jiongeze kwa awamu ya pili iliyoanza mwaka 2021 mpaka 2024 umeendelea kushirikiana na Idara ya Elimu Sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, umefanikiwa kuzifikia Shule 23 za Sekondari ambazo zina wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne.
COUNSENUTH kwa kushirikiana na Idara ya Elimu Sekondari ya Wilaya ya Tunduru imetekeleza mradi wa KIJANA JIONGEZE wenye lengo kuu la kukabiliana na changamoto za ufaulu wa na kuhusisha njia za kuwawezesha wasichana kuwa na stadi za maisha zitakazowasaidia kutambua uwezo wazo, kujiamini na kuwaandaa kwa ajili ya ajira na kujiajiri. Mradi huu umetekelezwakwa awamu zote mbili katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, kwa ufadhili wa MasterCard Foundation.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.