Tarehe 31 Agosti 2025, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ilizindua rasmi utoaji wa huduma katika zahanati ya kijiji cha Chawisi. Zahanati iliyojengwa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa gharama ya shilingi milioni mia mbili tisini na tatu, laki saba na hamsini elfu.

Ni siku ya furaha, siku ya historia, na siku ambayo wananchi wa Chawisi wataikumbuka daima. Kwa muda mrefu, walitembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya, lakini sasa huduma hizo zimeletwa mlangoni mwao. Furaha na shangwe za wananchi wa Chawisi zimesikika kila kona. Mwenyekiti wa kijiji hicho, kwa niaba ya wananchi wote, ametoa shukrani za dhati kwa serikali ya awamu ya sita kwa mradi huu mkubwa unaogusa maisha ya kila mmoja wao.

Lakini sio zahanati pekee – nyumba ya mtumishi pia ipo hatua za mwisho kukamilika, ishara ya kwamba huduma hii itakuwa ya kudumu na ya uhakika.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Wilfred Rwechungura, aliwataka wananchi wa Chawisi kujitokeza kutumia huduma zote zitakazotolewa katika zahanati hiyo. Aliwaelekeza wajawazito kuhudhuria kliniki pamoja na wenza wao, na watoto chini ya miaka mitano kupewa chanjo zote muhimu, dawa kinga na ushauri wa kiafya. Kwa kufanya hivyo, alisema, tutapunguza vifo vya uzazi na vifo vya watoto wachanga.
Aidha, Dkt. Rwechungura alisisitiza umuhimu wa kujikinga na magonjwa ya kuambukiza kama vile malaria, kifua kikuu, UKIMWI na homa ya ini. Vilevile aliwataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na Mpox, kwa kuzingatia kanuni za usafi: matumizi ya vyoo bora, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, na kuhakikisha maji ya kunywa ni safi na salama.

Mwisho, aliwakumbusha wananchi kuilinda miundombinu ya zahanati yao, huku akiwataka watumishi kutoa huduma bora na rafiki kwa kila mmoja, wakiwemo vijana.
Zahanati ya Chawisi si tu jengo jipya, bali ni ishara ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan – dhamira ya kupeleka maendeleo yanayoonekana hadi ngazi ya kijiji, dhamira ya kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Leo Chawisi inasherehekea, kesho itakuwa kijiji kingine, na hatua kwa hatua, Tanzania yote inasogea mbele – kwa afya bora, maisha bora na maendeleo yanayoguswa na kila mwananchi.
Hakika, Serikali ya Awamu ya Sita – Maendeleo Yanayoonekana, Matokeo Yanayoguswa!
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.