Bodi ya Afya na kamati za usimamizi wa vituo vya kutolea huduma ya Wilaya ya Tunduru imezinduliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mheshimiwa, Wakili Julius S. Mtatiro tarehe 27.10.2023. Uanzishwaji wa Bodi hii ikiwa ni kutimiza takwa la Sera ya Wizara ya Afya katika kuboresha utoaji wa huduma za Afya nchini.
Bodi ya Afya na kamati za usimamizi wa vituo vya kutolea huduma ya Wilaya ya Tunduru ilianzishwa Mwezi Januari 2023 huku ikifuata hatua zote za uanzishwaji, ikiwa na wajumbe 18, wakiwemo wataalamu wa afya, viongozi wa jamii, na wawakilishi wa wananchi.
Akizungumza Katika uzinduzi huo, Mh. Wakili Mtatiro, Alisema, Bodi hiyo itasaidia Halmashauri kusimamia ufanisi wa shughuli za afya na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Tunduru. Pia, Mh. Wakili Mtatiro alisisitiza Bodi kusimamia nidhamu za watumishi wa afya na kuhakikisha kwamba wanatekeleza majukumu yao kikamilifu.
“Kazi ya bodi hii ni kusimamia fedha za Halmashauri ziende katika vipaumbele vilivyopangwa na Halmashauri pamoja na Baraza la madiwani, na pale ambapo Bodi ikigundua kuna fursa ambayo inaweza ikapanua wigo wa mapato msisite kushauri na kusimamia hilo Alisema, Mnapaswa kuhakikisha fedha zetu haziendi sehemu tofauti, madawa yanaponunuliwa yaende kwa walengwa yasitoke vituo vya kutolea huduma kwenda maduka ya watu binafsi.
Aidha, Mhe. Mtatiro alitilia mkazo juu ya wananchi kupatiwa Elimu ya mfuko wa Huduma za Afya (CHF) iliyoboreshwa, ikiwa ni hatua muhimu katika kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma za afya kwa wananchi wa kipato cha chini.
Uzinduzi wa Bodi hiyo ni hatua muhimu katika kutekeleza sera ya Wizara ya Afya ya kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini. Bodi hiyo inatarajiwa kuchangia katika kuboresha ufanisi wa shughuli za afya katika Halmashauri, pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Tunduru.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.