WANANCHI WILAYANI TUNDURU WAPATA ELIMU YA BIMA.
Miaka mingi iliyopita kipindi cha wakoloni wakati wananchi wengi nchini Tanzania na duniani kote wakiwa katika wimbi la kupata hasara za upotevu na uharibifu wa mali zao na kupata matatizo makubwa ya kiafya ambapo matibabu yake ni vigumu kuyamudu kutokana na kughalimu pesa nyingi ulitokea ufumbuzi wa matatizo hayo kwa kuanzisha mifumo ya ukataji bima.
Katika kuhakikisha Elimu ya bima inawafikia wananchi wengi zaidi, Mamlaka ya usimamizi wa shughuli za bima nyanda za juu kusini wametoa Elimu ya masuala ya bima wilayani Tunduru hapo jana. Akifungua mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na mamia ya wananchi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya Tunduru Bw. Eberhad Halla aliwasihi wananchi kujiunga na makampuni ya bima mbalimbali za afya, biashara, mali zao ili kupunguza makali ya maumivu pindi wanapopata majanga ya mali hizo.
Naye meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima nyanda za juu kusini Bi. Consolata M. Gabone alianza kwa kufafanua kwa kina maana ya bima kuwa, ni mkataba wa biashara ambapo mtu mmoja, ama kikundi cha watu, taasisi au shirika, kwa mujibu wa sheria, huchukua jukumu la kutoa ahadi ya kulipa hasara itakayotokana na uharibifu wa mali, upotevu wa mali, kifo, au hasara nyinginezo anazopata mkataji wa bima anayeingia mkataba na mtoaji wa bima yaani yule anayekubali kuwa tayari kufidia hasara hiyo. Akiendelea kueleza aina na umuhimu wa Bima, meneja huyo alisema "
Bima imegawanyika katika makundi mawili:-
i)Bima za muda mrefu: Hizi ni bima ambazo muda wake ni zaidi ya mwaka mmoja na kuendelea, mfano bima za maisha na
ii)Bima za muda mfupi; hizi ni bima ambazo ni mikataba ya muda usiozidi mwaka mmoja, mfano: bima za magari, moto, meli, ndege, wizi na ajali."
"Bima zote za muda mrefu na muda mfupi ni muhimu sana maishani mwetu kwani kuna bima za aina nyingi mfano bima za vyombo vya moto, bima za biashara, bima za afya, bima za maisha, bima za kilimo, bima za moto na bima za ajali kazini. Bima hizi zinasaidia kwanza kabisa kulinda biashara kutokana na majanga yasiyo tarajiwa, pili kulinda wafanyakazi kutokana na majanga mbalimbali, tatu kulinda afya ya mkataji wa bima, nne kulinda wateja ambao wanaweza kudhurika katika eneo la kazi na mwisho kuleta mazingira bora ya kufanya kazi katika biashara." Alisema Bi. Consolata Gabone
Bwana Kurenje Mbura ambaye ni afisa mafunzo ya bima alisema serikali kutokana na umuhimu wa bima na baadhi ya matatizo yaliyokua yanajitokeza kwenye utoaji wa huduma za bima mwaka 2009 serikali ilifanya marekebisho ya sheria ya bima na kuunda sheria mpya ya bima namba 10 ya mwaka 2009 ndipo kikaundwa chombo maalumu kinachojitegemea kikiwa chini ya Wizara ya Fedha na Uchumi cha kusimamia na kudhibiti masuala ya bima kiitwacho Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima (Tanzania Insurance Regulatory Authority "TIRA") inayoongozwa na Kamishina wa Bima Nchini. Chombo hiki kiliundwa ili Kuweka mazingira mazuri ya ushindani katika soko la bima hapa nchini, Kusajili wadau mbalimbali wanaofanya biashara za bima (Kama vile, Makampuni ya Bima,Madalali wa Bima,Wakadiriaji hasara za mali na Ajali; na Mawakala wa Bima), Kuindeleza sekta ya bima na kuifanya kuwa kichocheo cha kukua kwa uchumi, Kuweka viwango vya kiutendaji wa kibiashara ndani ya soko la bima, Kuhakikisha soko la bima hapa nchini haliingiliwi, Kuhakikisha kuwa huduma zitolewazo ni za gharama nafuu na zinazomlenga mteja, Kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusiana na huduma za bima na Kutoa elimu ya bima kwa umma.
Ili kuhakikisha kuwa elimu na huduma ya bima inawafikia wananchi wengi zaidi nchini Tanzania mamlaka hiyo imegawa kanda za usimamizi. Kwa Zanzibar ofisi ipo Zanzibar na kwa Tanzania bara mamlaka ina ofisi tano ambazo ni Kanda ya Nyanda za Juu Kusini- Mbeya, Kanda ya Ziwa- mwanza, Kanda ya Kati- Dodoma, Kanda ya Kaskazini- Arusha na Makao Makuu ya Mamlaka ya Bima Dar es Salaam.
Kwa sasa wananchi wanaweza kupata taarifa mbalimbali za mamlaka ya usimamizi wa shughuli za bima na kuhakiki stika za bima za vyombo vya moto kirahisi zaidi kupitia simu zao za mkononi kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi, kupakua App ya TIRA MIS na njia ya mwisho ni kutumia mtandao wa http//mis.tira.go.tz
Bw. Kurenje mbura Afisa mafunzo ya bima akijibu maswali yahusuyo bima (aliyesimama) na kulia kwake ni meneja wa mamlaka ya usimamizi wa bima nchini kanda ya nyanda za juu kusini Bi.Consolata Gabone
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.