Mpango wa kunusuru kaya maskini wilayani Tunduru umebadili maisha ya wanufaika wilayani Tunduru ukilinganisha na walipokuwa wanaishi kabla ya mradi huu kuanza kutekelezwa mwaka 2014.
Hayo yamebainishwa na mratibu wa mradi wa kunusuru kaya maskini (TASAF) Ndg Muhidin Shaibu wakati alipotembelea kijiji cha Namakambale kuona maendeleo ya wanufaika wa mradi huo.
Alisema " tangu mradi umeanza mwaka 2014 kumekuwa na mabadiliko makubwa yamefikiwa kwenye kaya hizo ikiwemo kuongezeka kwa wanafunzi shuleni,kuhudhuria kliniki na kaya kuwa na uhakika wa kupata milo mitatu kwa siku tofauti na siku za nyuma hivyo kupungua kwa kiwango kikubwa tatizo la udumavu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano".
Aidha baadhi ya wanufaika wa mpango huo wameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za ruzuku ambazo zitawasaidia kuwajengea uwezo wa kiuchumi kwa kuanzisha biashara na kuwapatia kipato cha kila siku.
Akitoa ushuhuda wa namna mpango huu ulivyomuwezesha kujikwamua kiuchumi Bi Mwajuma Kassima mnufaika kutoka kijiji cha Misufini Kata ya Namiungo amesema, licha ya TASAF kumwezesha kupata kipato pia ameweza kujenga nyumba ya vyumba vitatu anayoishi na familia yake." kabla sijaanza kupokea fedha za Tasaf nilikua na maisha duni naishi kwenye nyumba ndogo iliyojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi jambo lililosababisha kudharaulika mbele ya jamii,lakini baada ya kuingia kwenye mpango nimekuwa mtu mwenye amani katika maisha yangu na heshima kubwa".
Naye Bi Asha Mponda mnufaika kutoka kijiji cha Namakambale alisema TASAF imemwezesha kujenga nyumba ya kisasa,kusomesha watoto na kuweza kuanzisha mradi wa ufugaji ambapo mpaka sasa ana jumla ya Mbuzi nane, kumuongezea kipato na kuheshimika katika kijiji chao.
Kwa upande wa Mtendaji wa Kata ya Namakambale Bi.Hadija Lukanga alisema, kata hiyo ina kaya 391 waliopo katika mpango wa kunusuru kaya maskini kati ya hizo zipo kaya wapo ambao wameanzisha vikundi vya kuweka na kukopa pamoja na biashara ndogo ndogo.
Alimalizia kwa kutoa shukrani kwa serikali na kusema kuwa TASAF imesaidia sana kuboresha maisha ya wananchi wa kata hiyo kwani hata kiwango cha umaskini kimepungua sambamba na mahudhurio makubwa ya watoto shuleni ambao wote wanakwenda wakiwa na sare na mahitaji yote muhimu ikilinganisha kabla ya mpango kuanza utekelezaji.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.