Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Simon Chacha ametoa maagizo hayo katika Kikao cha kujadili hali ya udahili wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kilichofanyika leo tarehe 10.02.2025, katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tunduru. Mhe. Chacha alitoa agizo kuwa watoto wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza wakaandikishwe shule mara moja.
Mhe. Chacha, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho, ameagiza kuwa wazazi na walezi wote ambao hawajapeleka watoto wao kuandikishwa shule wanapaswa kukamatwa kuanzia kesho tarehe 11.02.2025. Alisisitiza kuwa kumpeleka mtoto shule ni takwa la kiserikali na ni kwa manufaa ya mtoto mwenyewe. Pia, wazazi/Walezi ambao wameandikisha watoto wao shule za nje ya Wilaya ya Tunduru wanapaswa kutoa taarifa haraka iwezekanavyo.
“Hatuwezi kuendelea kufanya kazi hii kwa kubembelezana, ni muda sasa wa kuchukua hatua za kisheria, hii sio kwa manufaa yao tu bali ni kwa ajili ya taifa kwa ujumla” aliendelea kuzungumza kuwa “Wanasheria wetu watatusaidia kuhakikisha tunafuata taratibu zote za kuwafikisha mahakamani wale wote watakaokaidi agizo hili”
Aidha, Mkuu wa Wilaya ameagiza kuwa zoezi la kuwafuatilia na kuwabaini wazazi/walezi ambao hawajaandikisha watoto wao kidato cha kwanza likamilike ndani ya wiki mbili, kuanzia leo tarehe 10.02.2025, baada ya hapo zoezi hili litafuatia kwa wazazi/walezi ambao hawajapeleka kuwaandikisha watoto wao Shule ya awali na Msingi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Ndg. Chiza C. Marando alizungumza kuwa kila Mzazi/Mlezi wa Mtoto aliyefauru kujiunga na kidato cha kwanza anapaswa kumpeleka kuandikishwa.
“Watoto wote waliofauru wapelekwe shule kuandikishwa,kukosekana kwa sare za shule isiwe kikwazo cha kumnyima mtoto haki yake ya msingi, apelekwe akaandikishwe huku mzazi/mlezi akiendelea kutafuta namna ya kumpatia mtoto wake sare hizo”
Akihitimisha kikao hicho Mhe. Chacha alisisitiza kuwepo kwa ushirikiano baina wataalamu wa ngazi zote, kufanya hivyo kutawarahisishia hata katika zoezi la usimamizi wa Miradi ya maendeleo, ambapo alizungumza kuwa ataanza kuzungukia miradi yote ili kuhakikisha inakamilika ndani ya muda ulioelekezwa.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.