Na: Theresia Mallya, Tunduru DC
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Juma Zuberi Homera amesema kuwa ni wajibu kwa kila kiongozi kusikiliza na kutatua kero za wananchi ili kupigia hatua za maendeleo yao.
Mhe. Homera ameyasema hayo wakati wa ziara ya ukaguzi wa mashamba ya Ufuta, kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Tarafa za Namasakata na Lukumbule zilizopo katika jimbo la Tunduru Kusini.
Akijibu kero za uhaba wa maji katika Tarafa ya Lukumbule na Namasakata Mhe. Juma Homera alisema kuwa amesikia kilio cha muda mrefu cha wananchi juu ya uhaba wa maji katika vijiji vingi vya wilaya hiyo.
Aliongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Help for Underserved Community (H.U.C) wanachimba visima vya maji katika majimbo yote mawili ya Tunduru Kusini na Kaskazini ili kupunguza tatizo la maji katika halmashauri ya Tunduru.
Aidha Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Help for Underserved Community (H.U.C) kwa sasa inaendelea kufanya utafiti katika vijiji vilivyosalia ili kufanya uchimbaji wa visima vya maji vilivyosalia kuanzia mwezi Mei 2019.
Ambapo vitachimbwa visima 11 katika Kata ya Tuwemacho, viwili viwili katika vijiji vya Nasya, Namasalau na Chemchemi, na visima vitano kijiji cha Tuwemacho ambapo visima vitatu 3 ni mchango wa Mkuu wa wilaya na visima viwili mchango wa mfuko wa kuchochea maendeleo ya Jimbo la Tunduru Kusini.
Mhe. Homera aliendelea kusema kuwa ili kuongeza uzalishaji na wananchi kufanya kazi za kujiletea maendeleo ni vyema huduma za jamii kuwepo karibu kama maji, ili kufikia lengo la serikali la upatikanaji wa maji vijijini kwa asilimia 85 ifikapo 2020.
Hata hivyo upatikanaji wa maji safi na salama katika halmashauri ya Tunduru hadi kufikia Aprili 2019 ni asilimia 69 kwa maji mjini na asilimia 68.5 maji vijijini.
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.