Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Eng. Maryprisca Mahundi (Mb), amekagua miradi ya maji kwa siku mbili kuanzia tarehe 20-21 mwezi Novemba katika wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa maji katika mji wa Tunduru, Mhe.Eng.Mahundi amepongeza juhudi zinazofanywa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) katika kutekeleza mradi huo. Hata hivyo, ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya usambazwaji wa maji kwa maeneo ya mjini Tunduru, amemtaka Meneja wa Usambazaji wa Maji Tunduru mjini, kushughulikia changamoto zote zinazokwamisha upatikanaji wa maji na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.
Katika ziara hiyo, Mhe. Eng. Mahundi alikagua mradi wa maji uliopo katika Tarafa ya Nalasi unaosimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA). Mradi huo unagharimu shilingi Bilioni 2.4 na una uwezo wa kuhudumia wananchi kutoka vijiji 7. Ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 70, ambapo hadi kufikia sasa, kilomita 3 kati ya 24 za mabomba ya kusafirisha maji kutoka kwenye chanzo cha maji hadi vijijini zimeshakamilishwa. Aidha, vituo 9 kati ya 24 vya maji vimeshajengwa.
Akizungumza na wananchi, amesema kuwa Serikali ina dhamira ya kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata maji safi na salama. Hata hivyo, amesisitiza kuwa ni lazima wananchi wote wanashirikiana na kuelimishana juu ya umuhimu wa kutunza miundombinu ya maji. Pia, kuwahakikishia kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi wote.
“Nimeona changamoto nyingi katika usambazaji wa maji kwa maeneo ya mjini. Kuna maeneo mengi ambayo hayapati maji kwa wakati. Nimemuagiza Meneja wa mamlaka ya maji mjini Tunduru (TUUWASA) kushughulikia changamoto zote pamoja na kuzitafutia ufumbuzi. Pia, anapaswa kuandika ripoti juu ya changamoto hizo haraka iwezekanavyo,” alisema Mhe.Eng. Mahundi.
Ziara hiyo ya Mhe.Eng. Mahundi ni mwendelezo wa ziara zake za kukagua miradi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini. aliahidi kwamba Serikali itaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora ya maji.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.