Naibu Katibu Mkuu, Elimu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ,Dkt. Charles Msonde, amefanya ziara ya kikazi wilayani Tunduru, Mkoani Ruvuma, kukagua miradi ya maendeleo sekta ya Elimu.
Katika ziara hiyo, Dkt. Msonde alionyesha kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa miradi hiyo ambayo ipo katika hatua ya umaliziaji. Alisema kuwa miradi hiyo itasaidia kuboresha upatikanaji wa elimu bora kwa wanafunzi wa wilaya ya Tunduru. Pia, ametoa maagizo kwa viongozi wa shule hizo na kamati zinazosimamia miradi hiyo, kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilishwa kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Dkt. Msonde alikagua ujenzi wa shule mpya iliyopo katika kata Tuwemacho, mradi uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 560, Mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 mwezi Novemba mwaka huu. Pia, alikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni na matundu ya choo katika shule za sekondari Masonya, Tunduru na Nandembo.
Alisema kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya Elimu ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata elimu bora na yenye ubora. Alisisitiza kuwa suala la ujenzi uaminifu na uadilifu, mahitaji ya miundombinu ni mengi lakini wataalamu na wasimamizi wote wanapaswa kusimamia kikamilifu kuhakikisha miradi yote inakamilika.
“Miradi hii ikikamilika kwa wakati na ubora itasaidia kupunguza umbali kwa watoto wetu waliokuwa wakilazimika kutembea kwa muda mrefu kwenda mahali shule ilipo, Maendeleo yanaanzia kwenye Elimu” Alisema Dkt. Msonde “Lengo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha anaboresha miundombinu yote ya Elimu ili watoto wapate elimu karibu na katika mazingira bora”.
Baada ya kukagua miradi hiyo, Dkt. Msonde aliridhika na utekelezaji wake, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya maendeleo, na pia aliwapongeza wabunge wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Daimu Mpakate (Jimbo la Tunduru Kusini) na Mh. Hassan Kungu (Jimbo la Tunduru Kaskazini) pamoja na madiwani wote, kwa kuendelea kutekeleza ilani ya Chama cha mapinduzi. Vilevile, alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru Ndg. Chiza C. Marando pamoja na timu yake ya wataalamu na kamati za ujenzi kwa kusimamia vyema utekelezaji wa miradi hiyo.
Ukaguzi huu wa miradi wa mara kwa mara unasaidia kutambua mapungufu yoyote katika utekelezaji wa miradi, na hatua za kurekebisha mapungufu hayo huchukuliwa mara moja. Ukaguzi huangalia utekelezaji wa miradi ya maendeleo hiyo kwa kuzingatia mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uwiano wa gharama na kazi iliyofanyika, ubora wa vifaa na kazi zilizofanywa, muda wa utekelezaji wa mradi na matumizi sahihi ya fedha za mradi.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.