Theresia Mallya 03.10.2019
Katika kuhakikisha kuwa kanuni taratibu na miongozo inafuatwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 24, 2019 wasimamizi wasaidizi katika vituo wanatakiwa kusoma, kuelewa na kufuata miongozo na ratiba ya uchaguzi huo.
Hayo yamesemwa na katibu tawala Mkoa wa Ruvuma Profesa Riziki Shemdoe katika ufunguzi wa semina kwa wasimamizi wasaidizi ngazi ya Kata na Vijiji katika vituo vyote vya uchaguzi wa serikali za mitaa.
Akisoma taarifa ya maandalizi yaliyofanywa na Halmahauri ya wilaya ya Tunduru Kaimu Afisa uchaguzi Ndg Abdul Kasembe amesema kuwa msimamizi wa uchaguzi amekua akifuata ratiba ya uchaguzi kama ilivyo katika mwongozo wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019, aidha Halmashauri ina jumla ya vituo vya uchaguzi wa serikali za mitaa 1179 ambavyo vitatumika katika uchaguzi huo.
Akiongea na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ambao pia watendaji wa Kata na Vijiji wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wawezeshaji kwa waandikishaji wa orodha ya wapiga kura, Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Profesa Riziki Shemdoe ambaye pia ni Msimamizi mkuu wa Uchaguzi mkoa alianza kwa kuwapongeza watendaji wote kwa kazi nzuri wanayofanya ya usimamizi hasa katika eneo la ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri.
Msimamizi wa uchaguzi Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mwalimu Anderson Mwalongo akitoa maekelezo kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa katika mafunzo kwa uwezeshaji kwa waandikishaji wa orodha ya wapiga kura.
Prefesa amesema “niwapongezeni kwa usimamizi mzuri wa mapato kufikia 59% ya makusanyo ya ndani licha ya 51% ya makusanyo yaliyokuwa yameelekezwa kwenye ushuru wa zao la korosho kutokuwepo, hongereni sana” lakini pia mnapaswa kuendelea kusimamia mapato , kuwa waaminifu, na kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia Sheria,Taratibu na Kanuni za utumishi wa Umma.
Pia niwatake muendelee kutoa ushirikiano katika kutekeleza majukumu, lakini pia niwaombee muendelee kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika maeneo yenu ya utawala ili kuleta tija kwa wananchi mnaowasimamia.
Vilevile Profesa Shemdoe aliwataka wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa kufanya maamuzi sahihi katika kila hatua wanayochukua katika masuala yote ya uchaguzi wa serikali za mitaa.
Katika picha ni wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Kata na Vijiji wakipewa mafunzo elekezi ya namna ya kusimamia shughuli za uchagauzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.
Profesa Shemdoe ameendelea kusisitiza wasimamizi kuhakikisha kwamba wanasoma kanuni na mwongozo wa serikali za mitaa, kuzielewa kujua nini kifanyike na kufuatwa katika taratibu za uchaguzi, pia mzingatie ratiba ya uchaguzi wa serikali za mitaa inaelekeza nini.
Wasimamizi wasaidizi mnatakiwa kuwepo katika vituo vyenu vya kazi muda wote wa uchaguzi ili kuondoa mikanganyiko ambayo inaweza kujitokeza wakati wote wa maandalizi hadi kufanyika kwa uchaguzi novemba 24, aidha kwa wasimamizi wa uchaguzi wasaidizi hakutakuwepo na ruhusa au likizo mpaka uchaguzi utakapokwisha na kutowepo doasari katika eneo lako la uchaguzi.
Hata hivyo alimalizia kwa kuwapongeza Mkurugenzi Mtendaji halmashauri Ndg Gasper Balyomi pamoja na msimamizi wa uchaguzi Halmashauri ya Tunduru Mwalimu Anderson Mwalongo kufanya maandalizi vyema na kufuata ratiba iliyopo katika mwongozo wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka 2019.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.