“Naomba unapokwenda kuitembelea shule usikubali kwenda kama hujui unakwenda kufanya nini”hayo yalisemwa na Afisa Elimu wilaya mwalimu Anderson Mwalongo alipokutana na maafisa elimu kata katika ukumbi wa klasta kujadili utekelezaji wa maagizo ya afisa elimu mkoa juu ya mikakati ya kuboresha sekta elimu wilayani Tunduru.
Mwalimu Mwalongo alisema ili kuboresha kiwango cha ufaulu katika halmashauri ya wilaya ya Tunduru ni lazima maafisa elimu kata kufanya kazi kwa weledi na kurudisha nidhamu ya mwalimu katika shule zilizopo katika kata wanazosimamia.
Pia alitoa maelekezo ya namna bora ya kufaya usimamizi wa shule za msingi na sekondari zilizopo katika kata zao ili kuhakikisha kuwa walimu wanafundisha kulingana na sera ya elimu ya mwaka 2003, kuwa na maandalio, na kutoa mitihani ya kila wiki na mwezi ili kuwapima wanafunzi.
Mwalimu Mwalongo aliendelea kutanabaisha kuwa Maafisa Elimu Kata wanatakiwa kuwa na mpango kazi (work Plan) wenye chachu au tamaa ya kufikia lengo fulani katika shule zote zilizopo ndani ya Kata husika, kufanya kazi zenye matokeo chanya wakati wa kutekeleza sera na miongozo mbalimbali ya elimu inayotolewa na serikali na kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu iliyo bora na sio bora elimu.
Maafisa Elimu Kata kutoka wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru wakifuatilia kwa karibu maagizo ya Ofisa Elimu wilaya Mwalimu Anderson Mwalongo ambaye hayupo katika picha katika kikao cha kazi kilichofanyika ukumbu wa klasta ya Mlingoti mapema leo hii, kwa ajili ya kuwakumbusha namna bora ya utendaji kazi katika kusimamia elimu wilayani Tunduru.
Aliendelea kwa kuwataka Maafisa hao kufanya kazi na kuepuka siasa na kufanya kazi zao kwa kuzingatia lengo alilojiwekea, “unapoenda kufanya usimamizi kwenye shule epuka maneno mengi, wewe sio mwanasiasa nenda kwenye lengo lako mara moja na pia muwe na tabia ya kuweka kumbukumbu ya ushauri na maagizo mnayotoa kwa wakuu wa shule mara mtembeleapo shule kuona maendeleo ya taaluma kwa wanafunzi” alisema Ofisa Elimu Msingi.
Pia aliwataka waratibu/maafisa elimu kata kuvaa viatu vyao pale mkuu wa shule anapokiuka maadili ya kazi ya ualimu, kanuni na taratibu za uendeshaji mzima wa sekta ya elimu katika shule yake kuweza kuwachukulia hatua za kidhamu, ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri, barua za onyo na hata kumuwajibisha pale anaposhindwa kutekeleza majukumu yake, kwa kufanya hivi kiwango cha ufaulu kitaongezeka.
Hata hivyo mwalimu Anderson Mwalongo alimalizia kwa kuwataka Maafisa Elimu Kata kuhakikisha KASIKI za kuhifadhia mitihani zinajengwa katika kila shule ya msingi iliyopo katika Kata anazosimamia, na kwa shule ambayo hawatajenga kasiki hizo mpaka kipindi cha mitihani, mkuu wa shule atapata gharama ya kusafirisha mitihani hiyo kwa shule jirani ambayo wana kasiki ya kutunza mitihani.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.