Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Dini Wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuzuia unyanyasaji wa kijinsia katika Mazingira yanayowazunguka.
Wito huu umetolewa katika semina iliyofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, ambapo viongozi hao walikutana kujadili ustawi wa jamii kupitia mshikamano wa madhehebu ya dini.
Mada kuu iliyowasilishwa katika semina hiyo ilihusu "Namna Bora ya Kuzuia Unyanyasaji wa Kijinsia katika Mazingira Yanayomzunguka Mwanadamu."
Akizungumza wakati wa semina hiyo, Meneja wa Mradi wa Kuimarisha Mshikamano Miongoni mwa Madhehebu Mbalimbali ya Dini, Ndg. Erick Gallawa, alisisitiza jukumu la viongozi wa dini katika kuzuia unyanyasaji wa kijinsia kutokana na nafasi yao kubwa ya kuaminika katika jamii.
Naye, Mwenyekiti wa mradi huo, Erasto Kitie, aliwapongeza viongozi wa dini kwa mawasilisho mazuri na kuwaomba kuendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia njia mbalimbali kama vile mashuleni, nyumba za ibada, na ofisi za serikali ili kujenga jamii bora.
Kwa upande wake, Mchungaji Torben Madsen, Katibu Mkuu wa International Aid Services kutoka Denmark, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na kusisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kusimama pamoja katika shughuli zao za kijamii ili kuendeleza amani na mshikamano katika jamii.
Mafunzo hayo yalifungwa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Ndg. Fadhili Chidyaonga, ambaye ni Mratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, ambaye alishukuru mradi huo kufika katika halmashauri ya Tunduru na kuelezea faida zilizopatikana kwa viongozi wa madhehebu ya dini katika kujifunza namna ya kushirikiana katika mambo mbalimbali.
Kwa upande wa viongozi wa madhehebu ya dini walioshiriki semina hiyo, Stephen Makina alisisitiza jukumu lao la kushirikiana na serikali katika kukemea unyanyasaji wa kijinsia kwa kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.