Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Adv, Julius S. Mtatiro, amehitimisha vikao vya kazi vya kufuatilia udahili wa kidato cha kwanza mwaka 2024
Akizungumza katika vikao kazi na Watendaji wa Kata,waratibu Elimu kata, Wakuu wa shule na watendaji wa vijiji, amewapongeza kwa juhudi zao za kuhakikisha wanafunzi wote wanapata nafasi za kuendelea na masomo yao ya Sekondari.
Ambapo mpaka kufikia Februari 05, 2024 asilimia 86 ya Wanafunzi wa kidato cha kwanza wamedahiliwa shule za sekondari na kufanya Takwimu kwa kila Tarafa kuwa, Tarafa ya Nakapanya asilimia 96.4, Tarafa ya Mlingoti asilimia 95.6, Tarafa ya Namasakata asilimia 88.4, Tarafa ya Nampungu asilimia 85.8, Tarafa ya Matemanga asilimia 81.1, Tarafa ya Lukumbule asilimia 79.4, na Tarafa ya Nalasi asilimia 78.7.
Mhe. Mtatiro amesema kuwa, amefurahishwa na kasi ya udahili katika kata nyingi, na amewataka Watendaji kuendelea na juhudi zao ili kuhakikisha asilimia 100 ya wanafunzi waliohitimu darasa la saba wanadahiliwa kidato cha kwanza,pia Mh. Mtatiro ameahidi kutoa ushirikiano wake kwa Watendaji wote katika kuhakikisha udahili unakamilika kwa mafanikio.
"Nimefurahishwa na maendeleo ya udahili katika wilaya yetu. Hii ni ishara ya juhudi kubwa zinazofanywa na Watendaji wetu katika kuhakikisha Watoto wote wanapata Elimu bora." Alisema Mhe. Mtatiro
Aidha, amewataka Watendaji kuunda mikakati ya ndani ili kuendelea kuhamasisha Wazazi na walezi kuwapeleka Watoto wao shule, na pia kutafuta suluhu kwa changamoto zinazokwamisha udahili. Baadhi ya changamoto zilizotajwa ni pamoja na baadhi ya Wanafunzi kutoka familia zenye mahitaji maalum, hasa wale wanaolelewa na bibi na babu waliozeeka sana baada ya wazazi kuwatelekeza, hawajapata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza. Baadhi ya wazazi kukimbilia mashambani na misituni kujificha ili wasipeleke watoto wao sekondari.
Kwa upande wao Watendaji wa Kata pamoja na vijiji wamehaidi kushirikiana na serikali ya Wilaya kuhakikisha asilimia ya Wanafunzi ambao bado hawajadahiliwa wataweza kudahiliwa kabla ya kufungwa kwa dirisha la udahili wa wanafunzi kidato cha kwanza.
Vikao kazi vilivyofanyika na Mkuu wa Wilaya vimetoa msukumo mkubwa kwa Watendaji wa kata katika kuhakikisha udahili wa kidato cha kwanza unakamilika kwa mafanikio. Kwa ushirikiano wa pamoja kati ya serikali na wananchi, wilaya ya Tunduru ina lengo la kufikia asilimia 100 ya udahili katika mwaka huu wa masomo.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.