Ofisi ya Usimamizi Maendeleo ya Ushirika Wilaya ya Tunduru imefungua Mikutano Mikuu ya kawaida ya vyama vya Msingi vya ushirika. Mikutano hii inajumuisha uchaguzi wa bodi mpya za vyama hivyo.
Ufunguzi huo ulifanyika katika Chama cha Msingi cha Ushirika Mtetesi (Mtetesi AMCOS) katika kata ya Mindu. Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa vyama vya ushirika, wanachama, na Viongozi kutoka ngazi mbalimbali za Serikali.
Katika mkutano huo, uchaguzi ulifanyika kuchagua bodi mpya ya kusimamia na kuongoza Chama cha Msingi cha Ushirika Mtetesi. Uchaguzi huo ulifanyika kwa mujibu wa utaratibu uliotolewa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), unaotaka vyama vyote vya ushirika kuendesha uchaguzi wa uongozi wa bodi mwaka huu 2024.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Afisa Ushirika (W) Tunduru Ndg. George N. Bisani aliipongeza bodi mpya iliyochaguliwa ya Chama cha Msingi cha Ushirika Mtetesi. Aliisisitiza bodi hiyo kutengeneza mikakati ya ndani ya chama ili kuweza kukiinua kiuchumi zaidi ya pale kilipo sasa.
Bw. Bisani pia aliitaka bodi mpya kuhakikisha Wanachama na Wakulima wanasajiliwa katika Mfumo Mpya wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU).
"Tugombane kuhusu maendeleo, ili tuzidi kuwaita wawekezaji katika chama chetu," alisema Bw. Bisani. "Kinachomvutia Mkulima kujiunga uanachama ni uadilifu wa uongozi."
Kwa upande wake, Mwenyekiti aliechaguliwa wa Bodi ya Chama cha Msingi cha Ushirika Mtetesi Bw. Adamu Rashidi Mpelela ameahidi kuonesha ushirikiano wa moja kwa moja kwa bodi iliyochaguliwa pamoja na wanachama ili kuweza kuinua chama kiuchumi.
"Sisi tumechaguliwa kutoka miongoni mwenu wanachama tunaomba ushirikiano wenu wa dhati katika kufikia mafanikio ya chama," alisema Bw. Mpelela.
Sambamba na hayo, Diwani wa Kata ya Mindu, Mhe. Richard Bazil Nakoko, ameisisitiza bodi iliyochaguliwa kubadili mwenendo wa chama ili kuweza kupata mafanikio, hasa katika uchumi wa chama hicho.
Mkutano huo ulihitimishwa kwa wito kwa viongozi wapya wa vyama vya ushirika kushirikiana na wanachama wao ili kuleta maendeleo ya vyama vyao na kuinua maisha ya wananchi.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.