Katika juhudi za kudumu za kulinda wananchi na mali zao dhidi ya migongano na wanyamapori, hasa tembo, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imeendelea kutoa mafunzo ya vitendo kwa wananchi wa vijiji vya Matemanga na Changarawe. Mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo wa kutumia uzio wa pilipili na vilipuzi kama njia bora za kuzuia migongano.
Mafunzo haya yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali ngazi ya Tarafa, Kata, kijiji pamoja na Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Matemanga, wote waliahidi kutoa ushirikiano wa kina ili mafunzo haya yaweze kuleta tija katika jamii na yafanikiwe ili kuepuka migongano baina ya binadamu na wanyamapori.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Bwana Dunia Almas, ambaye ni Kaimu Afisa Maliasili na Hifadhi ya mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, amewataka wananchi kuzingatia kwa makini mafunzo haya ili waweze kuyatumia katika maisha yao ya kila siku. Amesisitiza umuhimu wa kutenga maeneo maalumu ya kilimo ili kuepuka kuingia katika hifadhi za wanyamapori. Aidha, Bwana Almas amewakumbusha wananchi juu ya umuhimu wa kulima zao la pilipili, ambalo limeonekana kuwa na ufanisi katika kuzuia wanyamapori kuingia katika mashamba.
Mafunzo haya yaliandaliwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Hifadhi ya Taifa (TANAPA) na Pams Foundation. Ushirikiano huu unaonyesha dhamira ya pamoja ya kulinda mazingira na kuhakikisha kuwa wananchi wanaishi kwa amani na wanyamapori.
Mpaka sasa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ikishirikiana na wadau mbalimbali imefanya mafunzo katika vijiji 12, ambapo pamoja na mafunzo hayo pia imeweza kugawa vifaa ambavyo vitasaidia wananchi katika kupunguza migongano hiyo.
Serikali inaendelea kutoa wito kwa wananchi wote kuunga mkono juhudi hizi za kulinda mazingira na kuishi kwa amani na wanyamapori. Kupitia mafunzo haya, inatarajiwa kuwa idadi ya migongano itashuka na wananchi wataweza kuendelea na shughuli zao za kila siku bila wasiwasi.
Imetolewa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru,
Orpa Kijanda.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.