Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Komredi Oddo Mwisho, amefanya ziara ya siku tano mfululizo Wilayani Tunduru kuanzia tarehe 25- 29.07.2024. Ziara hii imekuwa na lengo la kuimarisha uhusiano kati ya viongozi na wananchi, kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Ujumbe wa ziara hii umekuwa ukiongozwa na Komredi Oddo mwenyewe, akiambatana na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Kamati ya Siasa Mkoa na Wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru ambaye amekuwa akiwakilishwa na katibu tawala wa wilaya ya Tunduru ndg. Milongo Sanga, Wabunge wa Majimbo yote ya Tunduru Mhe. Daimu Idd Mpakate na Mhe. Zidadu Kungu,waheshimiwa Madiwani, Mkurugenzi wa Halmashauri Ndg Chiza Marando na Wataalamu ambao wameshiriki kutoa taarifa za kiufundi na kusimamia utekelezaji wa miradi.
Moja ya shughuli kubwa katika ziara hii imekuwa ni ushiriki katika hafla za mapokezi ya fedha za miradi ya maendeleo katika kata mbalimbali ikiwemo Mtina, Mbati, Ngapa, na Nakapanya. Hafla hizi zimekuwa zikitoa fursa kwa wananchi kuona juhudi za serikali za kuleta maendeleo katika maeneo yao.
Aidha, Katika hotuba zake, Mwenyekiti amekuwa akitumia fursa hii kuzungumza na wananchi katika maeneo mbalimbali kama vile, Mlingoti, Matemanga (ambapo ndipo atamalizia Ziara yake katika Kata hii tarehe 29.07.2024). Katika mikutano hii, amekuwa akisikiliza na kutatua kero za wananchi. Pia, amekuwa akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo akiwahimiza kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa. Amesema kuwa uchaguzi huu ni fursa kwa wananchi kuchagua viongozi bora ambao wataweza kuwatumikia kwa uaminifu na kuwaletea maendeleo.
Vile vile, mwenyekiti alipata wasaa wa kuzungumza na wakuu wa Idara na vitengo wa Halmashauri, wakuu wa Taasisi mbali mbali katika Wilaya ya Tunduru. Aliwahimiza kujitahidi kutumia ujuzi na utaalamu wao katika kutatua kero za wananchi na kutimiza majukumu yao katika uadilifu ili kuwasaidia wananchi wa Tunduru.
Imetolewa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru,
Orpa Kijanda,
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.