Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Eng. Maryprisca Mahundi, amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa vijiji vya Mtina,Tinginya, Lipepo, Nalasi na Chilundundu wilaya ya Tunduru.
Mkutano huo ulilenga kusikiliza kero za wananchi kuhusu upatikanaji wa maji. Katika mkutano huo, wananchi walieleza kero mbalimbali wanazokumbana nazo, ikiwemo Ukosefu wa maji ya uhakika, hususani katika maeneo ya vijijini, Maji machafu ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu, na Uharibifu wa vyanzo vya maji.
Mhe. Eng. Mahundi aliahidi kuhakikisha kero zote zinafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo. Alisema kuwa Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maji katika wilaya ya Tunduru, na kwamba miradi hiyo itakapokamilika, itasaidia kutatua changamoto za maji kwa wananchi. Aliahidi kuagiza wataalamu watakaosaidia kuboresha miundombinu ya maji na kuhakikisha kuwa maji yanapatikana kwa uhakika.
"Nimesikia kero mnazokumbana nazo, nami naahidi kuungana na adhima ya serikali ya awamu ya sita chini ya Raisi wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha tunamshusha mama ndoo kichwani inatimia, " alisema Mhe. Eng. Mahundi.”Ninakwenda kuwaagiza wataalamu wangu kuhakikisha kwamba kila kijiji kinafikiwa na maji safi na salama”.
Aidha, Mhe. Eng. Mahundi alikemea wananchi wanaofanya shughuli za kilimo na ufugaji karibu na vyanzo vya maji kuacha mara moja. Alisema kwamba shughuli hizo zinachangia uharibifu wa vyanzo vya maji. Hivyo,alishauri kuwa wananchi wanapaswa kufanya shughuli hizo kuanzia umbali wa mita 60 kutoka kilipo chanzo cha maji.
Katika mkutano huo Mhe, Eng Mahundi alimpongeza meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Tunduru Eng. Maua Joseph Mgala, kwa kufanikiwa kusambaza maji maeneo ya vijijini kwa asilimia nyingi, vilevile kusimamia vyema na kuhakikisha mradi wa maji vijijini unakamilika kwa viwango na ubora wa juu.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.