Imefika miaka 26 tangu Muasisi wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aage dunia, lakini bado misingi, falsafa na dira aliyoiacha inaendelea kuwa mwanga unaoiongoza nchi kuelekea maendeleo endelevu.
Tangu enzi za kupatikana kwa Uhuru, Mwalimu Nyerere alihimiza Watanzania kudumisha umoja, amani na kujitegemea, akiamini kuwa maendeleo ya kweli yanapatikana pale wananchi wanaposhiriki moja kwa moja kuyajenga kwa kutumia rasilimali walizonazo.
Katika moja ya hotuba zake, Mwalimu Nyerere alisisitiza kuwa:
> “Maendeleo lazima yawaguse watu, yawasaidie kuinua maisha yao katika hali ya Uhuru, siyo ya utegemezi.”
Aliwahimiza Watanzania kutumia mali asili, ardhi, madini, gesi, misitu na utaalamu wa ndani kabla ya kutegemea wataalam kutoka nje, akiamini kuwa njia hiyo ndiyo itakayowezesha Taifa kusonga mbele kwa uhuru wa kweli.
Falsafa zake ziliweka msingi wa maendeleo tunayoona leo. Ndoto yake ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi sasa imetimia; Serikali inatekeleza majukumu yake yote kutoka mjini humo kama alivyotamani. Vilevile, maono yake kuhusu kilimo na viwanda yanaendelea kutekelezwa kupitia sera na mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongoza mapinduzi katika sekta hizo kwa lengo la kuinua uchumi wa wananchi.
Hayati Nyerere aliamini kuwa maendeleo hayana maana kama hayaleti mabadiliko katika maisha ya watu, jambo ambalo linaendelea kuzingatiwa hadi leo kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
Serikali imeendelea kutekeleza miradi mikubwa kama vile Reli ya Kisasa (SGR), Mradi wa Umeme wa Mto Rufiji, Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), pamoja na ujenzi wa shule, hospitali, barabara, bandari, viwanja vya ndege na meli mpya — yote ikiwa ni uthibitisho wa kuenzi fikra za Baba wa Taifa kwa vitendo.
Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (2020–2025) pia imeendeleza falsafa hizo kwa kusisitiza kujenga uchumi wa kitaifa unaowanufaisha Watanzania na kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi wote, si wachache.
Leo hii, tunapomkumbuka Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, tunatambua kuwa mchango wake haukuwa wa maneno pekee, bali ulikuwa wa vitendo vilivyojenga misingi imara ya Taifa.
Mwalimu, tutakukumbuka daima – kwa hekima zako, kwa maono yako, na kwa moyo wako wa kuwatumikia watu.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.