Afisa Elimu, Elimu ya watu wazima (DSAEO) wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru, Bi. Mariamu Magulima, amefanya kikao maalumu cha kuwapongeza na kuwatia moyo wanafunzi waliohitimu na wanaoendelea na masomo yao tarehe Decemba 05 katika kituo cha Mlingoti TRC wilayani humo.
Akizungumza katika kikao hicho Bi.Magulima,alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka watoto wa kike waliokatisha masomo yao kwa sababu mbalimbali, kuamua kuwarejesha shule ili kupata haki yao ya msingi ya Elimu, na pia aliwasisitiza wanafunzi hao kutokukata tamaa, aliwaomba kuwa mabarozi wazuri kwa wenzao ambao bado hawajajiunga na elimu hiyo,na kwamba bado wanayo nafasi ya kutimiza ndoto zao kupitia Elimu.
“Ninyi ni darasa ambalo lipo mikononi mwa serikali, kufanya mtihani wa kufuzu (Qualifying Test-QT) ni hatua kubwa sana katika kuelekea kutimiza na kuziishi ndoto zenu katika kupata elimu bora” alisema Bi.Magulima “kupitia ninyi tunataka kuona idadi ya wanafunzi wanaojiunga inaongezeka Zaidi,hata pale mnapokuwa mmehitimu elimu yenu msisite kufika katika ofisi zetu ili tuwapatie ushauri zaidi wa jinsi ya kujiunga na masomo ya elimu ya juu Zaidi”
Katika halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, mradi huu ulianza rasmi mwaka 2022 mwezi Januari, ambapo kituo cha Mlingoti TRC kilifanikiwa kusajili wanafunzi 19 na wote walifanya mtihani wa kufuzu (Qualifying Test-QT), wanafunzi wawili tu ndio walifanya vizuri na kufanikiwa kuingia hatua ya pili, yaani kidato cha III na IV, ambao mwaka huu (2023) wamefanya mtihani wao wa utimilifu wa kidato cha nne.
Aidha, mpaka sasa kituo cha Mlingoti TRC kimefanikiwa kusajili wanafunzi 15 wa hatua ya kwanza na wote wamekwisha fanya mtihani wa kufuzu (Qualifying Test-QT), wanafunzi hawa wataaanza masomo yao mwaka wa masomo utakaoanza Januari, 2024.
SEQUIP (Secondary education Quality Improvement Project), ni Miradi maalumu ya kitaaluma inayosimamiwa na OR-TAMISEMI chini ya Taasisi ya Elimu ya watu wazima, yenye lengo la kuwaendeleza wanafunzi wa kike waliokatisha masomo yao ya sekondari katika mfumo rasmi, kwasababu mbalimbali zikiwemo ujauzito, hali ngumu ya maisha, maradhi ya kudumu na nyinginezo. Aidha, Serikali inagharamia masomo ya wanafunzi hawa kwa asilimia zote.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.