Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Wakili, Julius S. Mtatiro ameongoza mdahalo wa kujadili mustakabali wa Wilaya ya Tunduru katika kilele cha maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wa Tanzania Bara.
Mdahalo huo ulihudhuriwa na viongozi wa vyama vya kisiasa, dini, wanafunzi, wazee maarufu na wakazi wa Wilaya ya Tunduru, ulilenga kuzungumzia mafanikio ambayo wilaya imeyapata kwa miaka 62 tangu Tanzania Bara kupata uhuru wake.
Pichani:Wanafunzi wakishiriki Mdahalo
Katika mdahalo huo washiriki walijadili masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Elimu, Afya, Kilimo, Maji na Miundombinu ya barabara. Pamoja na mafanikio yanayoendelea kupatikana kwa miaka 62 tangu Tanzania Bara ipate Uhuru wake, Wilaya ya Tunduru bado inahitaji kuwekeza Zaidi katika sekta ya kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula. Vile vile, wilaya ya Tunduru inaendelea kujenga na kuboresha upatikanaji wa miundombinu ya Elimu na afya ili kuwaandaa wananchi kwa maendeleo na pia uwepo wa huduma bora za afya.
Akizungumza mara baada ya kuongoza mdahalo huo Mhe. Wakili, Mtatiro alisema kwamba maadhimisho ya Uhuru Tanzania Bara huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kukumbuka historia ya harakati za kudai uhuru wetu toka kwa wakoloni na mchango wa viongozi wetu. Hivyo, kuna kazi kubwa katika kuhakikisha tunalinda Uhuru, umoja na mshikamano kwakuwa pasipo na mshikamano ni vigumu sana nchi kupata maendeleo.
“Tumekuwa na watoa mada kutoka idara ya Elimu msingi na Sekondari, Afya, kilimo, RUWASA na TARURA, wametupitisha kule ambako tumetokea, tulipo na tunapoelekea katika maendeleo kama Wilaya kwa miaka 62 ya uhuru wa Tanzania bara” alisema “Nchi yetu imepiga hatua kubwa ukilinganisha wakati ule inapata uhuru mpaka sasa tunatimiza miaka 62, tumepata maendeleo makubwa sana na tija imeongezeka katika sekta mbalimbali”
Aidha, Baada ya Mdahalo huo kumalizika Mhe. Wakili, Mtatiro alieleza umuhimu wa uhuru wa Taifa la Tanzania, alisema taifa letu linaongozwa kwa kufuata misingi ya kidemokrasia na kuzingatia uhuru wa wananchi wake. Wananchi waliahidi kufanya kazi kwa pamoja ili kushirikiana na serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais wa awamu ya sita, Mhe. Daktari Samia Suluhu Hassan katika kuboresha maisha ya wananchi wa Wilaya ya Tunduru.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.