Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Wakili Julius S. Mtatiro amefanya ziara ya siku tatu ya kikao kazi kuanzia tarehe 25-27 mwezi Januari 2024 kufuatilia hali ya udahili wa watoto shule za sekondari zilizopo wilayani Tunduru. Ziara hiyo ilihusisha Afisa Tarafa wote, watendaji kata, Afisa Elimu kata wote, na wakuu wa shule za Sekondari katika wilaya nzima.
Mhe. Wakili Mtatiro alieleza kuwa anasikitika kuona kuwa bado kuna idadi kubwa ya wanafunzi ambao bado hawajaandikishwa shule za sekondari. Aliwataka watendaji kata na Afisa Elimu kata wote kusimamia kikamilifu udahili wa wanafunzi katika kata zao.
Aliwataka watendaji kata kutengeneza utaratibu maalumu wa kuzifikia familia na wazazi au walezi wote ambao bado hawajapeleka watoto shule na kuhakikisha watoto wote ambao hawajaandikishwa wanaanza masomo mara moja. Wakifanya kazi kwa kushirikiana wataweza kuboresha hali ya udahili wa watoto shule za sekondari katika wilaya ya Tunduru.
Pichani:Baadhi ya Wakuu wa Shule, Afisa Elimu kata na Watendaji wa Kijiji wa Wilaya ya Tunduru.
“Ninashangazwa na kusikitishwa na idadi ndogo ya wanafunzi ambao wameandikishwa shuleni mpaka sasa, Watendaji kata na Afisa Elimu kata Shirikianeni na polisi kata ili kuhakikisha watoto wote ambao hawajaandikishwa shule mpaka sasa wanapelekwa shule” Alisema “Msipochukua hatua za haraka kuhakikisha watoto hawa wanapelekwa shule, mimi nitawachukulia hatua za kisheria ninyi”.
Mhe. Wakili Mtatiro alitoa agizo kuwa watoto wote ambao hawajaandikishwa watafutwe na waandikishwe shuleni, kwani elimu ni haki yao ya msingi. Alisisitiza kuwa mzazi yoyote ataye kiuka agizo lake achukuliwe hatua mara moja.
Aidha, aliwataka Wakuu wa Shule kuandaa utaratibu mzurii wa kuwapokea wanafunzi ambao utawasaidia kuwafuatilia kwa ukaribu kulingana na taarifa zao, aliongezea kuwa wanapaswa kushirikiana na serikali ya kijiji katika zoezi la kuwapokea wanafunzi hao ili kusiwepo na changamoto yoyote.
Ziara ya Mhe. Mkuu wa Wilaya inaonyesha kuwa serikali inatambua umuhimu wa elimu ya sekondari, ziara hiyo pia inaonyesha kuwa serikali inachukua hatua za kuboresha upatikanaji wa elimu ya sekondari kwa watoto wote wa Tanzania, kwa kuhakikisha inatengeneza miundombinu bora inayowezesha wanafunzi kupata masomo yao katika mazingira bora.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.