MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Ndugu Chiza Marando, amefanya ziara ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo tofauti ya wilaya ya Tunduru, kwa lengo la kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Marando aliwataka mafundi, Mafundi Ujenzi na wasimamizi wote wa miradi kuhakikisha wanaharakisha utekelezaji wa kazi kwa kuzingatia viwango vilivyokubaliwa, huku akisisitiza kuwa miradi yote inapaswa kukamilika na kukabidhiwa rasmi ifikapo tarehe 01 Machi. Alitoa maelekezo kuwa kazi ifanyike usiku na mchana ili kufikia muda uliopangwa.

Aidha, alitoa onyo kali kuwa hatovumilia uzembe wa mtaalamu au fundi yeyote atakayesababisha ucheleweshaji wa kukamilika kwa miradi hiyo, na kusisitiza kuwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wote watakaokiuka maagizo hayo, ili kulinda thamani ya fedha za umma na maslahi ya wananchi.
Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa katika ziara hiyo ni pamoja na ujenzi wa shule ya awali na shule ya msingi katika Kijiji cha Majimaji, ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi Ruanda, ukamilishaji wa zahanati zilizopo katika vijiji vya Sauti Moja na Songambele, pamoja na mabweni yaliyopo katika Shule ya Sekondari Nakapanya ambayo kwa sasa tayari yanatumika.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru katika kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuhakikisha inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa manufaa ya wananchi wa Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.