Mradi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na ofisi ya Walimu katika Shule ya Msingi Magomeni iliyopo katika kata ya MajiMaji Wilayani Tunduru unaendelea kwa kasi.
Akizungumza na viongozi wa kijiji cha Magomeni, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Ndg. Chiza Marando alipotembelea kukagua maendeleo ya mradi huo leo tarehe 01.12.2023, ameisisitiza kamati ya ujenzi, wanakijiji wote kushirikiana na wataalamu kuhakikisha mradi huo unakamilika kikamilifu.
Mradi huo unaogharimu kiasi cha shilingi milioni 56 , Unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu ili kuruhusu wanafunzi kutumia madarasa hayo ifikapo mwezi Januari mwaka wa masomo 2024.
Aidha, Ndg. Marando amekemea utoro uliokithiri wa wanafunzi wa shule hiyo, ametoa wito kwa walimu na watendaji wa kijiji hiko kuhakikisha wanafuatilia kwa ukaribu wanafunzi wote ambao ni watoro sugu na wazazi ambao hawawapeleki watoto wao kujiandikisha na elimu ya msingi.
“Madarasa haya yatakamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi wa 12 ambapo mwezi Januari madarasa hayo mapya yataanza kutumika, wekeni utaratibu wa kuunda sheria ndogo ambazo zitawasaidia kuwafuatilia wazazi ambao hawapeleki watoto kujiunga na elimu ya msingi” alisema “Serikali ina wajibu wa kuhakikisha inatimiza majukumu yake ipasavyo, lakini jamii hasa wazazi wanapaswa kuhakikisha wanaisaidia serikali katika kutimiza majukumu hayo, ikiwa ni pamoja na kuandikisha watoto kujiunga na elimu ya msingi”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha magomeni ameahidi kuhamasisha wananchi kushiriki kwa kila hali kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili kuondoa adha ya wanafunzi kusongamana darasani.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.