MADIWANI WANAWAKE WAWAFUNDA NANDEMBO SEKONDARI.
Umoja wa Waheshimiwa Madiwani Wanawake wilaya ya Tunduru, ukishirikiana na idara ya Maendeleo ya jamii, ustawi wa jamii Pamoja na Dawati la Jinsia na watoto, wamefanya ziara katika shule ya Sekondari Nandembo Februari 08, 2024.
Lengo kuu likiwa kuzungumza na watoto wa Kike masuala mbalimbali yawahusuyo, hasa katika umri waliopo , ambapo mada mbali mbali zilizungumzwa na Wataalamu na Waheshimiwa Madiwani kwa ujumla.
Wakizungumza na Wanafunzi hao , Waheshimiwa Madiwani waliwahimiza Wanafunzi kuzingatia sana Elimu na kuwa na nidhamu, na maadili mema wakati wote katika jamii inayowazunguka, waliwataka Wananfunzi hao kutojihusisha na Mahusiano ya kimapenzi kwani kufanya hivyo kutapelekea kuaharibu malengo yao ya baadae,Sambamba na ilo waliwataka kujiepesha zaidi na Mimba za utotoni
Kwa upande wao wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, walitoa Elimu kuhusu aina mbalimbali za ukatili, jinsi ya kujikinga na ukatili, na wapi pa kupata msaada iwapo watapata athari za ukatili,
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa wanawake Wilaya ya Tunduru, Bi. Fatu Jabari, alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kuwafikia vijana hasa Wanafunzi wasichana na kuwaelimisha kuhusu ukatili ili waweze kujikinga na pia kupambana na tatizo hili katika jamii.
"Tunajua kuwa ukatili ni tatizo kubwa linaloathiri wanawake na watoto wengi nchini Tanzania," alisema Bi. Jabari. "Kwa hiyo, ni muhimu kuwapa vijana maarifa na ujuzi wa kujikinga na ukatili na pia kupambana na tatizo hili."
Wanafunzi walifurahishwa sana na elimu waliyoipata na waliwashukuru madiwani hao kwa kuwajali na kuwapa maarifa muhimu. Waliahidi kuwa watatumia elimu hiyo kujikinga na ukatili na pia kuwaelimisha wenzao na jamii kwa ujumla.
Diwani wa Kata ya Nandembo Mhe. Omari Malipesa, aliwashukuru waheshimiwa Madiwani wanawake hao kwa kutembelea shule hiyo na kuwapa wanafunzi elimu muhimu.
"Elimu hii ni muhimu sana kwa wanafunzi wetu," alisema Diwani Malipesa. "Itawasidia kujikinga na ukatili na pia kuwawezesha kuwa na maisha bora ya baadaye."
Ziara hii ni sehemu ya kampeni ya Umoja wa wanawake Wilaya ya Tunduru ya kupambana na ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto. Kampeni hii inalenga kuwafikia wananchi wa Wilaya ya Tunduru na kuwaelimisha kuhusu ukatili na jinsi ya kupambana na tatizo hili.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.