Na: Theresia Mallya –Tunduru
Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma wametakiwa kutoa ushirikiano unaaostahili baina yao na watendaji wengine wa Halmashauri hiyo ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Juma Zuberi Homera wakati akitoa salamu za Serikali katika Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Robo ya Tatu uliofanyika leo katika ukumbi wa klasta ya Mlingoti wilayani humo.
“Madiwani tukimuachia kila kitu Mkurugenzi na Mkuu wa wilaya ndio wasimamie na nyie kukaa pembeni hatutaweza kuwasaidia wananchi wetu kujikwamua na umaskini, nawaombeni Waheshimiwa Madiwani, tuungane pamoja na tuzungumze lugha moja katika kuiendeleza Tunduru kwani ni yetu sisi sote”, Alisema Juma Homera.
Homera amewataka Madiwani hao kufanya kazi kwa kushirikiana na Watumishi na Viongozi wengine wa wilaya hiyo ili kuongeza kasi ya ukuaji wa kiuchumi ili kufikia malengo ya uchumi wa Kati ifikapo 2025
Mkurugenz Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Gasper Z.Balyomi akitoa ufafanuzi wa hoja ya ukusanyaji mapato katika Mkutano wa Baraza la Madiwani Robo ya Tatu ya Mwaka wa Fedha 2019 uliofanyika leo katika ukumbi wa klasta Tunduru Mjini.
Alisema kuwa wakati wa kuunganisha nguvu ya pamoja katika usimamizi wa mapato ndani ya Halmashauri na kuhakikisha hakuna mfanyabiashara anakwepa kulipa kodi lakini pia kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha Mkuu wa Wilaya huyo aliongeza kuwa katika Msimu wa Kilimo wa Mwaka 2019 Serikali kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko wakulima wa zao la Ufuta watanufaika kwa kuuza ufuta katika mfumo mpya wa stakabadhi ghalani kama walivyouza wakulima wa Mikoa ya Lindi na Mtwara Msimu wa Mwaka 2018.
Aliwajulisha madiwani Halmashauri kwa kushirikiana na Vyama vya Msingi watashirikiana katika usimamizi wa ununuzi wa zao utakaofanyika katika vyama vya msingi wilayani Tunduru.
Hata hivyo serikali kupitia bodi ya mazao mchanganyiko inajipanga kuona namna ya ununuzi wa mazao kama Karanga, Choroko,Mbaazi, Mpunga na Njugu kuwekewa mkakati wa kuingizwa katika mfumo wa stakabadhi ghalani ili yalete tija kwa wananchi.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Tunduru Ndg. Gasper Zahoro Balyomi aliwataka Waheshimiwa Madiwani kutoka Kata zote kushiriki katika zoezi la usimamizi wa ununuzi wa mazao mbalimbali kwani Halmashauri imebainisha vituo vya kununulia mazao katika vijiji na kata zenu.
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.