Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yamefanyika leo Desemba mosi, ambapo maadhimisho hayo kwa Mkoa wa Ruvuma yameadhimishwa Wilayani Tunduru.
Maadhimisho hayo yaliambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo upimaji wa VVU na kifua kikuu, utoaji wa elimu ya afya ya uzazi na Lishe, na utoaji wa huduma za ushauri nasaha na kupima pamoja na Michezo mbalimbali ikiwemo Mpira wa Miguu.
Akizungumza mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani , Mhe.Wakili, Julius S. Mtatiro , ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, aliwataka wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kuendelea kujikinga na maambukizi ya VVU kwa kutumia njia salama za kujikinga zinazoshauriwa na wataalamu wa Afya.
“Maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi bado ni tatizo kubwa katika Mkoa wetu huu wa Ruvuma,” alisema “Wanaume tunapaswa kuhudhuria vituo vya afya ili kuweza kutambua afya zetu, Ni wajibu wa kila mwananchi kutambua afya yake ili aweze kujikinga na maambukizi na vile vile kuwalinda wengine”.
Aidha, akisoma taarifa ya mganga mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Daktari, Louis chomboko ya ugonjwa wa UKIMWI mkoani humo, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Bi. Mariamu Juma, alisema kuwa, asasi za kiraia zuchukue fursa ya kuelimisha na kuhamasisha watu kupitia huduma za afya kufanya ubunifu, kujenga uaminifu, kufanya ufuatiliaji na utekelezaji wa sera na afua za huduma mbalimbali na kusimamia uwajibikaji wa kila mmoja wetu.
Pichani: Ni Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa, Bi. Mariamu Juma, akisoma taarifa ya mganga mkuu ya ugonjwa wa UKIMWI mkoa wa Ruvuma.
Takwimu zilizosomwa katika taarifa ya mganga mkuu wa mkoa wa Ruvuma zinaonyesha kuwa, Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa 14 yenye asilimia kubwa ya maambukizi ya VVU kitaifa ukiwa na una asilimia 5.6, ambapo kiwango cha maambukizi kitaifa ni 4.7 kwa matokeo ya viashiria vya UKIMWI Tanzania yam waka 2016/2017. Aidha, kiwango hiki cha maambukizi kimepungua kutoka asilimia 7 mwaka 2011.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ikiwa ni “Jamii iongoze kutokomeza UKIMWI”, kauli mbiu hii inaangazia umuhimu wa kutoa nafasi kwa jamii kushika hatamu katika kutokomeza UKIMWI.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.