Kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa afua za lishe ngazi ya wilaya kimefanyika tarehe 30.07.2024 katika ukumbi wa klasta kata ya Mlingoti. Kikao hiki kiliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Simon Chacha na kilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Tunduru Ndg. Chiza Marando, wakuu wa idara na vitengo, na watendaji wa kata.
Kikao kililenga kutathmini maendeleo yaliyofanywa katika utekelezaji wa mkataba wa afua za lishe, kubaini changamoto zinazoikabili sekta ya lishe, na kupanga mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma za lishe katika wilaya.
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Chacha aliwapongeza watendaji wa kata kwa juhudi kubwa walizoziweka katika kutekeleza mkataba wa afua za lishe. Alieleza kuwa amefurahishwa na mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza udumavu katika baadhi ya kata.
“Endeleeni kuelimisha wananchi kujisimamia wenyewe hasa kwenye masuala ya Lishe bora, wasisubiri mpaka serikali ije ifanye” alisema “Wajitahidi kupambana kwa ajili ya afya zao wenyewe ili kuondoa hali ya udumavu”.
Mhe. Chacha alimpongeza Mtendaji wa kata ya Nakapanya Bi. Leocadia Mponda kwa ufanisi wake katika utendaji kazi wa maswala ya Lishe, pia, Bi. Leocadia alikabidhiwa cheti na kiasi cha shilingi 100,000 kama motisha ya kufanya kazi kwa bidii.
Pichani ni Mhe. Chacha akimkabidhi Cheti cha pongezi Bi. Leokadia Mponda.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya alibainisha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya. Aliwataka watendaji kuendelea kuimarisha ushirikiano ili kuweza kuondoa kabisa tatizo la udumavu katika wilaya. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuelimisha jamii kuhusu masuala ya lishe bora, kwani Mkoa wa Ruvuma unaojulikana kuwa na viwango vya juu vya udumavu licha ya kuwa na uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula.
Imetolewa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru,
Orpa Kijanda,
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.