Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo wilayani Tunduru, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), ujenzi wa Shule mpya, maabara, majengo ya Tehama, mabweni,na vyoo. Ziara hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mhe. Hairu Hemed Musa, na iliambatana na waheshimiwa Madiwani ambao ni wajumbe wa kamati hiyo.
Akizungumza katika majumuisho ya Ziara hiyo Mhe. Hairu amewaomba wananchi kujitolea kushirikiana na kamati za ujenzi ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati, pia, amewaagiza wataalamu kuhakikisha Shule Mpya zinakamilika kwa wakati ili kuruhusu zoezi la usajili na kuanza kupokea wanafunzi ifikapo mwezi Januari mwakani.
“Miradi hii ikamilike kwa viwango na kwa muda uliopangwa,timu nzima ya wataalamu na kamati za ujenzi, Wananchi wahamasishwe ili washiriki ujenzi wa miradi”. Alisema. “Tumegundua mapungufu kadhaa katika utekelezaji wa baadhi ya miradi, na hatua za kurekebisha mapungufu hayo tumeagiza zifanywe haraka ili kuendana na muda uliowekwa kukamilisha miradi”.
Kamati ilitoa agizo Miradi yote ya ikamilike kwa wakati, ili kuruhusu huduma kuanza kutolewa kwa wananchi, ukaguzi huo ni muhimu ili kuhakikisha kuwa miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia viwango.
Baada ya kukagua miradi hiyo, Kamati iliridhika na utekelezaji wake. Kamati iliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya maendeleo, na pia kamati iliwapongeza wataalamu pamoja na kamati za ujenzi kwa kusimamia vyema utekelezaji wa miradi hiyo.
Ukaguzi huu wa miradi wa mara kwa mara unasaidia kutambua mapungufu yoyote katika utekelezaji wa miradi, na hatua za kurekebisha mapungufu hayo huchukuliwa mara moja. Ukaguzi huangalia utekelezaji wa miradi ya maendeleo hiyo kwa kuzingatia mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uwiano wa gharama na kazi iliyofanyika, ubora wa vifaa na kazi zilizofanywa, muda wa utekelezaji wa mradi na matumizi sahihi ya fedha za mradi.
Imeandaliwa na Orpa Kijanda, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.