Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Tunduru Gasper Zahoro Balyomi wakati alipotembelea na kukagua ujenzi wa bwalo la chakula linalojengwa katika shule ya sekondari ya Nandembo iliyopo wilayani Tunduru
Serikali imetoa jumla ya shilingi Milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa Bwalo la chakula na Ukumbi wa Mikutano katika shule ya Sekondari Nandembo yenye kidato cha kwanza hadi sita,mradi uliotakiwa kukamilika tangu Mwezi Mei,hata hivyo hadi sasa ujenzi huo haujakamilika na huko katika hatua ya msingi jambo linalo leta wasiwasi kama kazi hiyo inaweza kumalizika.
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao ,baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo Rashid Ali na Bashiru Yacob wamesema, kwa sasa wanapata tabu kubwa kila unapofika muda wa chakula na wanatumia miti iliyopo shuleni hapo jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa maisha yao.
Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi Christopher Simkoko akimuonesha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tunduru Gaspar Balyomi ujenzi wa Bwalo la chakula na ukumbi wa mikutano unaojengwa katika shule ya sekondari Nandembo
Aidha,wamemuomba fundi aliyepewa jukumu hilo kuhakikisha anaongeza kasi ya ujenzi ili likamilike kwa wakati ili wanafunzi wapate sehemu nzuri na salama kwa ajili ya chakula na hata ukumbi wa mikutano.
Bashiru Yacob alisema, kula chakula chini ya miti ni hatari kwani wanaweza kupata vimelea vya magonjwa mbalimbali kama Tumbo na kuharisha kutokana na uzembe unaofanywa na fundi aliyekabidhiwa kazi ya ujenzi wa mradi huo.
Kwa upande wake,Mkuu wa shule hiyo ambaye ni katibu wa kamati ya ujenzi Mwalimu Mary Ndunguru alisema, wamepokea shilingi Milioni 100 kwa ajili ya mradi wa Bwalo na ukumbi wa mikutano hata hivyo ambapo mradi huo ulitakiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Mei,lakini umechelewa kukamilika kwa muda muafaka kutokana na mifumo ya fedha na fundi kushindwa kufanya kazi yake kwa wakati.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru Komred Gaspar Balyomi akikagua ujenzi wa Bwalo la chakula na Ukumbi wa Mikutano unaojengwa katika Shule ya Sekondari Nandembo wilayani Tunduru,hata hivyo ujenzi huo uliotakiwa kukamilika Mwezi Mei Mwaka huu upo katika hatua ya msingi kutokana na fundi wake kushindwa kukamilisha kazi hiyo kama ilivyokusudiwa.
Alisema, hadi sasa wametumia shilingi milioni 17 kati ya shilingi Milioni 100 na fedha zilizobaki shilingi milioni 83 ambazo ziko Benki, hata hivyo kuchelewa kukamilika kumewaathiri sana wanafunzi wake ambao wanatumia kivuli cha miti kwa ajili ya kulia chakula na kufanya mikutano ya kitaaluma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru Gaspar Balyomi akiwa katika eneo la mradi huo ametoa maagizo ya mradi huo kukamilika ndani ya mwezi mmoja kwa kuzingatia ubora na viwango.
Gasper alisema "natoa siku thelathini mradi kwa fundi Keneth John mradi huu uwe umekamilika, naomba mfanye kazi usiku na mchana ili kumaliza kazi hiyo"
Alisema, mradi huo huko nyuma kwa asilimia 50 na kuna uzembe mkubwa umefanyika katika usimamizi wake na ameitaka kamati ya ujenzi kuhakikisha inapeleka vifaa vyote vinavyohitajika ili kazi iende haraka na wanafunzi waondokane na kero kula chakula chini ya miti..
MWISHO
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.