Halmashauri ya Wilaya Tunduru inatarajia kutumia bilioni 36,899,337,707.08 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020, kati ya fedha hizo bilioni 2,641,184,396.00 mapato ya ndani, ikiwa mapato halisi Tsh 2,033,064,396.00 na mapato ya ndani mengineyo ni Tsh 608,120,000.00, pamoja na hayo ruzuku ya mapato mengineyo na mishahara imepanga kutumia Tsh 29,910,702,566 na Tsh 4,147,450,745.08 zitatumika katika miradi ya maendeleo kutoka serikali kuu.
Akiwasilisha rasimu ya bajeti ya mwaka 2019/2020 mbele ya baraza la madiwani kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Afisa Mipango halmashauri ya Tunduru Ndg Jumanne Mwankhoo alisema maandalizi yamezingatia vipaumbele vilivyotajwa katika mwongozo wa bajeti ya serikali za mitaa kwa mwaka 2019/2020.
Vipaumbele vya bajeti ni kukamilisha miradi viporo ili kuongeza upatikanaji wa huduma hususani katika sekta za afya na elimu, kutenga fedha kwa ajili ya huduma za lishe na mapambano dhidi ya maambikizi ya VVU na UKIMWI na kuwekeza katika miradi yenye mwelekeo wa vyanzo vya mapato hasa katika sekta ya kilimo na biashara.
Halmashauri imezingatia mwongozo wa taifa wa kutenga bajeti kwa ajili ya makundi maalum ikiwa walemavu asilimia 2, maendeleo ya wanawake 4 % na vijana 4%.
Hata hivyo alimalizia kuwasilisha bajeti mbele ya baraza la madiwani kwa kutoa mchanganuo wa matumizi ya makusanyo ya ndani, ikiwa Tsh 813,225,758 zitatumika katika miradi ya maendeleo itakayotekelezwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020, na tsh 1,219,838,638 kwa matumizi mengineyo. “lakini bajeti yetu ni pungufu kwa asilimia 15.5 ya mwaka 2018/2019 kutokana na kutojumuishwa kwa bajeti ya maji na baadhi ya program kama SEDEP, ASDP na LGCDG kumalizika muda wake” alisema kaimu afisa mipango.
Baraza la madiwani walipokea rasimu ya bajeti iliyowasilishwa na kuijadili na kutoa Baraka ili iwasilishwe katika ngazi nyingine za maamuzi kwa ajili ya utekelezaji,na kuomba serikali kuwasilisha fedha za miradi kwa wakati ili kukamilisha miradi pendekezwa kwa wakati.
Aidha mwenyekiti wa halmashauri ya Tunduru Ndg Mbwana Mkwanda Sudi aliwataka madiwani kushiriki katika zoezi la usimamizi na ukusanyaji wa mapato na kuibua vyanzo vipya vya mapato ili kuweza kufikia lengo la serikali la kila halmashauri kukusanya asilimia 80.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.