Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imefanya ziara ya kutembelea vijiwe vya maafisa usafirishaji wa bodaboda na bajaji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuwafikia vijana na kuwaelimisha kuhusu fursa mbalimbali za maendeleo zilizopo katika eneo lao.
Katika ziara hiyo, maafisa maendeleo ya Jamii walitoa elimu kwa vijana kuhusu fursa za kiuchumi ikiwemo mikopo ya asilimia 10 (10%) inayotolewa na Halmashauri kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Vilevile, vijana walielimishwa kuhusu fursa za mikopo ya vyombo vya moto, zikiwemo pikipiki na bajaji, inayotolewa na Benki za NMB na CRDB kwa masharti nafuu.

Aidha, Halmashauri ilitumia fursa hiyo kuwajulisha vijana kuhusu upatikanaji wa mafunzo ya muda mfupi ya udereva yatakayotolewa na Chuo cha Ufundi Nazareth Mbesa, Tawi la Tunduru Mjini (Biasi). Mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha vijana kupata vyeti vya udereva na hatimaye kumiliki leseni halali ili wawe madereva rasmi wanaotambulika kwa mujibu wa sheria.
Pia, ziara hiyo ililenga kusikiliza na kupokea changamoto pamoja na maoni kutoka kwa vijana, ikiwa ni utekelezaji wa adhma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwafikia vijana, kuwasikiliza na kushughulikia changamoto zao ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imeendelea kuwasisitiza vijana kutumia fursa zinazotolewa na Serikali ili kujikwamua kiuchumi na kuchangia katika maendeleo ya Wilaya na Taifa kwa ujumla.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.