Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Wakili Julius S. Mtatiro ameongea na wananchi wa Tunduru kupitia mkutano ya hadhara tarehe 29.01.2024 uliondaliwa katika tarafa ya Matemanga. Mkutano huo ulilenga kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi wa haraka.
Pichani: Baadhi ya wanakijiji wa Matemanga wakiwa katika Mkutano wa Hadhara.
Akizungumza katika mkutano huo Mhe. Wakili Mtatiro alisema kazi kubwa ya watumishi wa serikali ni kuwafikia wananchi ili kusikiliza kero na kuweza kuzitatua kwa kuzipatia suluhisho la kudumu. Sambamba na hilo, Mhe. Wakili Mtatiro aliwasisitiza wananchi kuwapeleka watoto shuleni.
Pichani: Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Wakili Mtatiro akizungumza na wananchi.
“Niwaombe wanajami, pelekeni watoto shuleni, hakuna maendeleo yatakayokuja kwa kuuza korosho pekee, hakuna kinachoendelezwa bila elimu” Alisema “Tutakaa tunalalamika kila siku kuwa hatupigi hatua kwenye maendeleo yetu pamoja na kwamba tunapata mazao ya kutosha, jamii itatoka kwenye umaskini pale ambapo elimu itathaminiwa”
Pichani: Wananchi wa Tarafa ya Matemanga wakitoa kero zao mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Wakili Mtatiro.
Aidha, Katika mkutano huo aliwasisitiza wananchi juu ya kuongeza mashamba ili kuweza kuongeza tija kwenye mazao. Pia, aliendelea kuwasisitiza wananchi kukodisha mashamba badala ya kuyauza ili kusaidia kupunguza migogoro ya ardhi na ufugaji wa mifugo kiholela.
“Tuwekeze nguvu kwenye kuandaa mashamba vyema yawe kwenye ubora ili uzalishaji wa mazao uwe juu, hii pia itasaidia kuongeza faida, kila unapohudumia shamba lako kikamilifu tarajia kupata mazao ya kutosha. Ni vigumu kuzuia mtu asiuze shamba lake lakini ni vizuri sana apewe elimu kabla ya kufanya maamuzi hayo” Alisema “Wakulima wengi hawajui siri ya kufanikiwa katika mazao hasa korosho, siri kubwa ni kuongeza mikorosho mipya ili kuweza kupata faida ya uhakika”.
Ziara hiyo ya Mkuu wa Wilaya imekuwa ya mafanikio makubwa kwani ameweza kusikiliza kero za wananchi mmoja mmoja na kuweza kuzitatua kwa wakati. Wananachi walipata wasaa wa kuelezea kero, hoja na mapendekezo yao ambayo walisaidiwa na kupatiwa ufumbuzi.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.