Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Wakili Julius S. Mtatiro, amefanya ziara ya kikazi kutembelea Shule ya Sekondari Ligunga. Katika ziara hiyo, amekagua miundombinu mbalimbali ikiwemo ya maji na vyoo.
Akiwa katika ziara hiyo, Mhe. Mtatiro alibaini uchakavu wa vyoo vinavyotumiwa na wanafunzi na vyoo vya walimu pamoja na shida ya maji. Ametoa agizo la ujenzi wa dharura wa vyoo hivyo kuanza kufanyika mara moja.
“Ninaagiza ujenzi wa dharura wa vyoo vya shule hii uanze mara moja,” alisema Mhe. Mtatiro. “Vyoo hivi ni muhimu kwa wanafunzi na walimu, na ni lazima viwe katika hali nzuri.”
Mhe. Wakili, Mtatiro pia alimuagiza Meneja wa Usambazaji Maji Vijiji (RUWASA), Eng. Maua Lugala, kuhakikisha wanashirikiana na TANESCO ili kufanya tathmini ya kuweza kusogeza maji karibu zaidi na shule hiyo.
“Shule hii inahitaji maji ya uhakika,” alisema Mhe. Mtatiro. “Ninaagiza RUWASA na TANESCO kufanya tathmini ili tuweze kusogeza maji karibu na shule hii.”
Meneja wa TANESCO Tunduru na Meneja wa RUWASA wote wawili wamepokea maelekezo na kuahidi kushirikiana na Halmashauri kuhakikisha Shule ya Sekondari Ligunga inakuwa na maji ya uhakika yatakayovutwa kwenye kisima cha shule na kurahisisha maisha ya wanafunzi shuleni hapo.
Akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo, Mhe. Mtatiro aliwasisitiza kuthamini elimu. Alisema kuwa elimu ndio msingi wa mustakabali mzuri wa maisha yao.
“Elimu ni muhimu sana kwa maisha yenu,” alisema Mhe. Mtatiro. “Ninyi ni vijana wa kesho, na elimu itawasaidia kufikia malengo yenu.”
Mhe. Wakili, Mtatiro pia aliahidi kuwa serikali itaendelea kujenga na kuboresha miundombinu na mazingira ya kujifunzia kwa Shule zote zilizopo katika Wilaya ya Tunduru.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, kwa mamlaka yake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, amemuahidi DC Mtatiro kuwa ataiongoza Halmashauri kuhuisha miundombinu ya shule ya Ligunga.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.