Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mheshimiwa Denis Masanja, amekabidhi hati za kimila 472 kwa wananchi wa Kijiji cha Ngapa. Mpango huu una lengo la kuleta utulivu na maendeleo kwa jamii. Utekelezaji wake unalenga kuondoa migogoro ya ardhi na kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi miongoni mwa wananchi, ambao mara nyingi wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ngapa, Dc Masanja alielezea kwamba, upatikanaji wa hati hizi unawaongezea wananchi ulinzi wa kisheria wa ardhi zao. Hati miliki za kimila zinatambulika kisheria, na hivyo kumpa mmiliki uwezo wa kudai haki zake endapo ardhi yake itavamiwa au kutumiwa na mtu mwingine bila ridhaa yake. Hii itawapa wananchi uhakika na amani ya moyo kwamba mali zao ziko salama na zinalindwa na sheria.
“Moja ya faida kubwa ya mpango huu ni kutatua migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiwakabili wakulima, wafugaji, na maeneo ya hifadhi. Kwa kuweka mipaka wazi na kurasimisha matumizi ya ardhi, zoezi hili linazuia mwingiliano usio wa lazima na hivyo kupunguza uwezekano wa kutokea kwa mizozo” Alizungumza DC Masanja “ Kupitia hati miliki za kimila, kila mwananchi anajua eneo lake na matumizi yake yamerasmishwa, jambo linalochangia amani na utulivu katika jamii zetu”.
Faida nyingine muhimu ni kwamba hati hizi zinaweza kutumika kama dhamana katika taasisi za kifedha, kama vile benki na taasisi nyingine za mikopo. Kwa kuwa na hati miliki ya ardhi, wananchi wanapata fursa ya kukopa fedha na kuanzisha au kukuza miradi yao ya maendeleo. Hii inachochea ukuaji wa kiuchumi kwa ngazi ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.
Aidha, Hati miliki pia zinatoa fursa kwa wamiliki kuzitumia kama dhamana mahakamani kwa ajili ya kesi mbalimbali, isipokuwa kesi za jinai. Hii inawasaidia wananchi kuwasaidia wapendwa wao katika matatizo ya kisheria bila kupoteza mali zao nyingine. Utoaji wa hati hizi unafungua milango ya fursa nyingi za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya, ndg Stephen Mpondo Afisa Mahusiano Jamii kutoka Hifadhi ya Taifa Nyerere (W),alizungumza kwamba, Jumla ya hati 2,783 zimetayarishwa kwa ajili ya vijiji nane vilivyopo katika Wilaya ya Tunduru vyenye mipango ya matumizi ya ardhi, kupitia mradi wa ERB unaosimamiwa na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere. Kati ya hati hizo, Kijiji cha Ngapa pekee kimepokea hati 472. Vijiji vingine vilivyofaidika ni Muhuwesi (hati 291), Mnazi Mmoja (hati 355), Liwangula (hati 312), Chawisi (hati 225), Jaribuni (hati 314), Matemanga (hati 156), na Ligunga (hati 658). Mpango huu unaonesha dhamira ya serikali ya kuboresha maisha ya wananchi wake kupitia urasimishaji wa umiliki wa ardhi.

Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.