Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Simon Kemori Chacha amewataka walimu wakuu na walimu wa michezo mashuleni kuhakikisha kuwa ratiba ya michezo zinazingatiwa na wanafunzi wapewe nafasi ya kushiriki michezo na sanaa katika shule zote za Msingi na Sekondari.
Agizo hilo lilitolewa wakati wa hafla ya ugawaji wa mipira kwa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Mkuu wa Wilaya amewataka walimu pia kuhamasisha wanafunzi kushiriki katika michezo mingine kama vile riadha, mpira wa kikapu, na netiboli. Ameongeza kuwa michezo ni muhimu kwa afya ya mwili na akili ya wanafunzi, na pia inawasaidia kukuza nidhamu na ushirikiano.
“tunatakiwa kuhakikisha vifaa hivi tunavitunza na kutumika kwa usahihi kama lengo la Serikali yetu katika kukuza michezo”. Alisema DC Chacha.
Afisa Michezo wa Halmasahuri ya Wilaya Tunduru, Ndg. Abilahi Namkopo, ameelezea Mipira hiyo ni zao la utekelezaji wa mpango wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) unaoitwa "Football for Schools". Mpango huo unalenga kukuza vipaji vya vijana wenye umri kuanzia miaka 8 hadi 17, ambao wengi wao wanapatikana mashuleni na jumla ya mipira 92 imegawiwa kwa shule sita za msingi na sekondari wilayani Tunduru.
Namkopo, ameongezea kuwa mpango wa "Football for Schools" unatoa fursa kwa vijana kuonyesha vipaji vyao vya mpira wa miguu na kupata mafunzo bora. Amewataka walimu kuhakikisha kuwa mipira hiyo inatumika vizuri na kuwashirikisha wanafunzi wote katika michezo.
Kwa upande wao Walimu wakuu na walimu wa michezo wameishukuru serikali kwa kushirikiana na FIFA katika kuinua sekta ya michezo nchini, hasa kwa vijana wenye umri mdogo. Wameahidi kutunza vifaa hivyo na kuvitumia kwa usahihi.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.