Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mheshimiwa Simon Kemori Chacha, amewaagiza viongozi katika kata na vijiji, pamoja na maafisa elimu kata kuhakikisha wananfunzi wanapata mlo wakiwa shuleni wakati wa masomo.
Amesema kuwa kufanya hivi kutaongeza ufanisi na umakini kwa wanafunzi katika masuala ya elimu, hasa katika kuongeza uelewa pale wanapofundishwa na walimu wao.
“Lishe ni kitu muhimu sana katika maisha ya kila mwanadamu , tunatakiwa kulichukulia hili suala kwa uzito wake katika maeneo yetu tunayoishi”.Alisema Chacha.
Chacha alitoa agizo hili wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa afua za lishe ngazi ya wilaya. Kikao hicho kilihudhuriwa na watendaji wa kata pamoja na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Aidha, Mkuu wa Wilaya alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi wa kata na vijiji, maafisa elimu, na jamii kwa ujumla katika kuhakikisha wanafunzi wanapata mlo bora shuleni. Alisema kuwa ushirikiano huo utasaidia kufanya kazi ya kuendeleza lishe bora katika Wilaya ya Tunduru.
Afisa Lishe wa Wilaya ya Tunduru, Ndugu, Martin Kigosi, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa lishe wilaya na jamii kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2024. Alisema kuwa wilaya imefanikiwa kutekeleza viashiria vya mkataba wa lishe kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa asilimia 93.1 robo ya kwanza, asilimia 96.7 robo ya pili, na asilimia 96.3 robo ya tatu.
Kigosi alipongeza jitihada zilizofanywa na viongozi wa kata na vijiji, maafisa elimu, na jamii kwa ujumla katika kutekeleza mkataba wa lishe. Aliwataka waendelee na jitihada hizo ili kuhakikisha Viashiria vyenye alama ya kadi nyekundu vinaondoka katika Wilaya ya Tunduru.
Kikao hicho kilimalizika kwa wito kwa viongozi wote kuhakikisha utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa ufanisi zaidi. Inaaminika kuwa mlo bora kwa wanafunzi utasaidia kuboresha ufanisi wao katika masomo na hatimaye kuleta maendeleo kwa wilaya na taifa kwa ujumla.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.