na Theresia Mallya 01/10/2019
Tundurudc.
Tatizo la Mimba mashuleni katika shule za sekondari wilayani Tunduru limekuwa changamoto kubwa sana katika utoaji wa huduma za elimu mashuleni licha ya jitihada zinazochukuliwa na serikali katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunza bado kuna nguvu ya ziada inatakiwa kuchukuliwa katika kutokomeza suala hilo.
Haya yamesemwa kwa masikitiko makubwa na mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Julius Mtatiro mapema leo wakati akizungumza na wazee wa wilaya hiyo katika maadhimisho ya siku ya wazee Duniani yenye Kauli mbiu inayosema "Tuimarishe Usawa Kuelekea Maisha ya Uzeeni" ambaye alikua mgeni rasmi.
Akitoa takwimu za Mimba kwa wanafunzi wa sekondari kwa kipindi cha miezi Miwili ya Agosti na Septemba Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa jumla ya wanafunzi 43 wamekatisha masomo wakiwa ni wa kidato cha kwanza hadi cha nne, ikiwa katika ya hao wanafunzi 25 walipatikana na mimba kwa kipindi cha mwezi Agosti pekee na mwezi agosti ni wanafunzi 19 hivyo kufanya jumla kuwa 43. Idadi hii ni kubwa sana kwani inaeudisha nyuma jitihada za serikali katika sekta ya elimu.
Baadhi ya wazee wa wilaya ya Tunduru wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe. Julius Mtatiro wakati akitoa hotuba katika maadhimisho ya siku ya wazee duniani ambayo yamefanyika kiwilaya katika ukumbi wa Klasta ya Mlingoti Mapema Leo.
Ameendelea kuwaeleza wazee kuwa kwa kipindi cha miezi 9 yaani kuanzia Januari hadi kufika julai 2019 jumla ya wanafunzi wa kike 119 wamekatisha masomo sababu ya kupata ujauzito angali bado wako shuleni, lakini kati ya kesi zote 119 Takwimu zinaonesha kuwa kesi nane tu ndio zilizofikishwa Mahakamani huku kesi nyingine 111 wazazi wakizimaliza wenyewe huko mitaani lakini kwa kipindi cha januari hadi septemba jumla ya wanafunzi wa kike waliokatisha masomo ni 162.
Julius Mtatiro ameendelea kusema kuwa sababu kubwa ya kuwa na wimbi la Mimba nyingi kwa wanafunzi ni watoto kukosa uangalizi wa wazazi kwani jamii inawaacha watoto kujihudumia wenyewe hasa kipindi cha kilimo wanaenda mashambani na kuwaacha peke yao nyumbani,wazazi kutojali wanafunzi wanapopata Mimba na mila na desturi hasa Unyago unachangia kwa kuwa na ongezeko kubwa la Mimba mashuleni.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe.Julius Mtatiro akisalimiana na Wazee alipofika katika ukumbi wa klsata mapema leo katika maadhimisho ya siku ya wazee duniani.
Vilevile wazazi na jamii kutozingatia maadili na malezi ya watoto nayo imekuwa ni chanzo kikubwa cha watoto kupata mimba angali bado wanafunzi. amesema "kati ya kesi 25 za mwezi Agosti watuhumiwa 16 wamefikishwa mahakamani h kufunguliwa jalada n zinaendelea katika mahakama ya wilaya huku watuhumiwa 15 kati ya 19 za mwezi septemba wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kuwatia wanafunzi Mimba, wazazi 6 wamefikishwa mahakamani kwa kushirikiana na watoto kutoa Mimba kwa kipindi cha mwezi agosti, huku zikiripotiwa zaidi ya kesi 3000 za utoaji Mimba kwa watoto katika kipindi cha Januari -Decemba 2018.
hata hivyo amewaomba wazee kufanya kazi ya malezi na maelekezo katika jamii kwani wazee ni hazina ya Taifa, pia kutoa mkazo katika elimu kwani maendeleo hayawezi kuja pasipo kuwa na elimu, hivyo amewaomba wazee na jamii ya Tunduru kwa Ujumla kuwekeza katika Elimu na kuachana na mila na desturi potovu ambazo zinawaiingiza mabinti wengi wadogo katika kupata mimba wakiwa bado wanahitaji kupata Elimu.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.