Baraza la Wafanyabiashara Tunduru Laanzishwa.
Baraza la wafanyabiashara ni chombo kilichoundwa kisheria kwa waraka wa Rais Na 1 wa mwaka 2001 na kuchapishwa katika Gazeti la serikali Na.691 tarehe 28 septemba mwaka 2001 ikiwa na lengo la kuunda jukwaa la majadiliano kati ya sekta binafsi na sekta ya Umma katika kila ngazi ya utawala ili kujadiliana jinsi ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Baraza la biashara lipo katika utaratibu wa kisheria kwani mwenyekiti wa baraza la kitaifa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli, katika ngazi ya mkoa ni mkuu wa mkoa na katika ngazi ya wilaya mwenyekiti wake ni mkuu wa wilaya husika.
Baraza hili limelenga katika kuboresha maeneo sita ya uboreshaji wa mazingira ya biashara katika matokeo makubwa sasa ambayo ni kuangalia upya mfumo wa kisheria na kitaasisi, Upatikanaji wa Ardhi na uhakika wa umilikishaji, Usimamizi na Uratibu wa shughuli za biashara, Utitiri wa kodi, tozo, na ada, Kuzuia na kupambana na Rushwa, sheria na stadi za kazi na Usimamizi wa mikataba na sheria za kazi.
Akiongea katika mkutano wa ufunguzi wa baraza la wafanyabiashara wilaya ya Tunduru mwenyekiti wa halmashauri Mh.Mbwana Mkwanda Sudi alisema wilaya ya Tunduru ina fursa nyingi sana za uwekezaji katika sekta ya Biashara, Kilimo, Afya, Elimu, Uchumi, utalii.
Mwenyekiti Mkwanda Sudi alisema katika sekta ya Utalii wilaya ya Tunduru ina vivutio vingi vya utalii ambavyo havijaendelezwa na endapo sekta binafsi itashiriki kikamilifu sekta ya utalii unaweza kutengeneza ajira za kutosha kwa jamii ya Tunduru na kufungua milango ya maendeleo katika wilaya yetu.
“Tunduru kuna nyao za viumbe vyote vinavyoishi duniani ambayo katika jiwe huko njenga ambayo naifananisha na safina ya Nuhu, kuna masalia ya majengo ya wapigania uhuru wa Msumbiji ya Masonya, vifuko alivyotumia Rais wa kwanza wa Msumbiji Samora Machel, Sultan Mataka na misafa ya watumwa wakitokea Msumbiji hadi Kilwa katika kipindi cha ukoloni na mengine mengi ambayo yanahitaji kuendelezwa” alisema mwenyekiti
Aidha meneja wa tanesco wilaya ya Tunduru Ndg Joseph K. Mtula alisema ni vyema halmashauri kuanza kutangaza fursa zilizopo katika wilaya kwa kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili kufanya jamii kuweza kujua fursa zilizopo ndani ya wilaya yetu.
Aliendelea kusema kuwa umeme umeenea katika maeneo mbali mbali ya wilaya ya Tunduru hali inayowezesha upatikanaji wa huduma ya umeme na wananchi kuweza kuanzisha viwanda hata maeneo ya kijiji kwa kule maeneo ambayo serikali imeshapeleka umeme.
Meneja TANESCO wilaya alitolea mfano wa mashine za kukoboa mpunga wilaya Tunduru ambazo kwa asilimia kubwa zipo katika tarafa ya mjini na kusema kuwa mashine hizi zinaweza kusimikwa pia vijijini kwa sababu umeme umefika maeneo mengi, serikali inaendelea kufunga umeme katika vijiji ambavyo havikuwa katika mpango umeme vijijini awamu ya pili, na barabara imeshafunguka hivyo kurahisha usafirishaji wa bidhaa hiyo.
Na kwa upande wa kaimu Afisa Madini wilaya Ndg Teddy Mataka alisisitiza kuwa Tunduru ina madini ya vito ambayo hupatikana tuu Tunduru katika nchi nzima ya Tanzania na pia kuna madini ya shaba (copper), na wajibu wa Halmashauri kushirikiana na taasisi za Umma, sekta binafsi kuona kuwa fursa hizi tunatangaza na kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza katika madini yetu.
Wajumbe wa baraza la biashara walisisitiza elimu kutolewa kwa wafanyabiashara wadogowadogo na vikundi vya wajasiriamali ili kuweza kuhakikisha kuwa baraza hili ilinasimama na kufikia malengo ya serikali ya kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2025 na agizo la viwanda 100 kwa kila mkoa linafanikiwa.
Hata wajumbe walisisitiza juu ya utwaaji wa ardhi na umilikaji ili waweze kutumia hati hizo katika kuomba mipoko katika taasisi za kibenki, na ujenzi wa hosteli kwa ajili ya wanafunzi kutokana na shule nyingi za sekondari za kata hazina hosteli hivyop wanafunzi kuhangaika makazi.
Halmashauri ya Wilaya Tunduru
Anuani ya Posta: 275, TUNDURU
Simu: + 255-025-2680004
Simu ya Nununu:
Barua Pepe: info@tundurudc.go.tz
Hakimiliki©2019 Halmashauri ya Wilaya Tunduru.Haki zote zimehifadhiwa.